2014-12-22 09:15:07

Askofu!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo! Kwa mara nyingine tena karibu tuendelee kuzipitia hati za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, tukiwa na lengo la kuhuisha ujumbe wake na kuuleta katika maisha ya Kanisa la nyumbani. RealAudioMP3

Tukumbuke kwamba Mtaguso huu ndio uliotoa dira mpya ya Kanisa tunayopaswa kuiishi sasa. Ndio maana, tunasihi na kusisitiza sana, tuzisome hati zake, tuufahamu, ili kweli tuwe wanakanisa hai.

Leo tunaitazama hati ya Mtaguso ambayo ni agizo linalohusu Utume wa Maaskofu katika Kanisa, ijulikanayo kwa lugha ya kilatini kama Christus Dominus, maana yake Kristo Bwana. Kabla ya kusema juu ya nafsi ya Askofu kama Wakili wa Kristo katika kundi alikokabidhiwa, ebu tuone mgawanyo wa maaskofu tulio nao katika Kanisa Katoliki.

Kwanza kabisa tunao Maaskofu-Jimbo. Hawa ni wakuu wa Makanisa Mahalia (yaani Majimbo). Ndiye anayehusika na kuwajibikia masuala yote ya kichungaji katika Jimbo, huku akisaidiwa na Makleri, Watawa na Waamini Walei. Na katika Jimbo kuna Askofu-Jimbo mmoja tu. Hata kama jimbo likawa kubwa namna gani, mwenye hadhi ya askofu Jimbo anakuwa mmoja tu, ndiye mwenye Mamlaka na Madaraka ya kitume katika Jimbo.

Chini yake, kuna Maaskofu Waandamizi. Askofu mwandamizi ni yule ambaye huteuliwa na Mama Kanisa, anatenda kazi ya kulichunga kundi chini ya maelekezo ya Askofu jimbo, lakini huyu anakuwa na uwezo wa kurithi Kiti cha Askofu Jimbo endapo Askofu Jimbo atakuwa nje ya madaraka kwa sababu iwayo yoyote.

Chini zaidi kuna Maaskofu Wasaidizi. Hawa humsaidia Askofu Jimbo katika shughuli za kichungaji za jimbo. Wanaweza wakawa maaskofu wasaidizi wanaoshughulika na vitengo maalumu, kwa mfano mmoja aweza kuwa Askofu Msaidizi anayeshughulika na maswala ya vijana tu katika jimbo, au akawa anashughulika na wakimbizi tu, au majeshi tu na mambo mengine kama hayo. Na palipo pengi Askofu msaidizi huwa ndiye Makamu wa Askofu. Ila tofauti na maaskofu waandamizi, Askofu msaidizi hana haki ya kurithi Jimbo, endapo kiti cha Askofu Jimbo kinakuwa wazi.

Na tena kuna Maaskofu wale wanaofanya kazi katika Ofisi Mbalimbali za Kiti cha Kitume, (Roma). Hawa nao wamegawanyika katika makundi kadhaa. Wapo Maaskofu, Maaskofu Wakuu na Makardinali. Humsaidia Baba Mtakatifu katika shughuli za kila siku za kulichunga Kanisa la Mungu. Na Baba Mtakatifu naye ni Askofu wa Roma, mwenye Mamlaka juu ya Jimbo la Roma na kila jimbo duniani.

Kinachowaunganisha hao wote licha ya kuwa na mgawanyo huo ni DARAJA TAKATIFU. Maaskofu wote wapo katika urika mmoja. Kwa daraja ya Uaskofu, wao ni Waandamizi wa Mitume, wanarithi baraza lote la mitume. Na Baba Mtakatifu peke yake, yeye ni Wakili wa Kristo duniani na mrithi wa Mtume Petro na Mchungaji Mkuu wa Kanisa lote duniani. Hadhi ya Daraja ya Uaskofu kama sakramenti ni ileile. Tofauti ni katika Madaraka na Mamlaka.

Maaskofu waliowekwa kuwa wachungaji wa Majimbo yetu, kwa namna ya Kitaali-Mungu, ndio wachungaji wakuu katika jimbo, wanaotuchunga sisi kwa jila la Kristo Bwana. Kristo Bwana, anafanya kazi ndani mwao, na kwa njia yao, ANATUFUNDISHA, ANATUTAKASA NA ANATUONGOZA, kuelekea makao ya milele. Maaskofu wetu, Wanaendeleza kazi ya Kristo duniani. Wao ndio wanaobeba dhamana ya wokovu wa roho zetu. Wanatekeleza agizo la Kristo ‘chunga kondoo wangu’. Na kondoo hao ndio sisi waamini.

Maaskofu hao wanapatikanaje? Katika Kanisa letu, Askofu hajazi fomu ya kugombea! Hapigiwi kura ya huru na wazi!! Zaidi tena, Askofu hapatikani kwa sababu ya akili zake nyingi au elimu kubwa au umaarufu wake, hasha!! Katika Kanisa letu kuna namna ya siri inayoongozwa na hekima ya kimungu ya kumpata Askofu. Kuna vigezo vingi sana na vigumu mno, vinavyosimamiwa na sheria ya pekee ya Kanisa, inayoongoza mchakato mzima hadi kumpata Askofu. Mchakato huo ni wa siri kubwa sana.

Kwa taratibu maalumu na kwa namna ya siri sana, hupendekezwa mapadre ambao wanastahili mbele ya macho ya Mungu kushika wadhifa wa Askofu. Nao hao kisha kupendekezwa, ofisi zinazohusika na kwa namna zilizowekwa na sheria ya Kanisa, huchunguzwa kwa kina na mapana na kwa muda mrefu sana. Na uchunguzi huo huwa ni wa siri mno, ili kweli kuweza kumpata mtu anayestahili kukabidhiwa dhamana ya wokovu wa roho za kundi la Mungu katika Jimbo.

Baada ya taratibu zote kukamilika, na mchujo mkubwa sana kufanyika, hubakizwa majina matatu ya wale wanaoonekana kustahili zaidi. Majina hayo hupelekwa kwa Baba Mtakatifu. Naye, na ni yeye tu (bila kushauriwa au kushawishiwa na mtu yoyote), kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu humchagua mmoja kati ya hao watatu, na kwa uhuru na mamlaka aliyonayo, humtangaza kuwa askofu wa jimbo fulani. Si rahisi, ndiyo maana daima tunaomba sala za waamini na watu wote ili Mungu atupatie wachungaji wa kutuongoza, kutulisha kwa neno na sakramenti ili tusaidiwe kuishi kitakatifu.

Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, sisi kama waamini, tunachotakiwa ni kusali kwa moyo, kuomba Mungu atupatie hao wachungaji wakuu. Lakini pia tunazidi kuwaombea amani na usitawi ili wafanye kazi vyema. Leo mahali pengi tunashuhudia ambavyo wachungaji wa roho zetu wanavyonyanyaswa na kudhulumiwa hata uhai wao.

Ulimwengu uliojifunika blanketi la uovu na dhambi, hauwataki kabisa wachungaji wetu kwa sababu wanakemea dhambi na uovu. Ni juu yetu sisi kuwaombea, kuwalinda ili wasipatwe na mawaa. Wanahitaji sala zetu hasa kipindi hiki ambapo shetani anajua anachokifanya, ‘anapiga wachungaji wetu ili sisi kondoo tutawanyike’!!

Tuwaombee wachungaji wetu wasipigwe na yule mwovu! Na hata wakitikiswa wasianguke!. Pamoja na zawadi nyinginezo zote, sala ndiyo zawadi nzuri zaidi na kubwa kwa ajili ya maaskofu wetu. Katika sala za familia, jumuiya ndogondogo, tusisahau kuwaombea maaskofu wetu. Tunapoomba sadaka ya misa kwa ajili ya nia mbalimbali, tusisahau kuwaombea maaskofu wetu.

Lakini wajibu msingi kabisa ambao unatoa ushirikiano chanya kwa maaskofu wetu ni Usikivu na utii wetu sisi kama waamini. Kanisa letu moja, takatifu, katoliki na la mitume, huongozwa kwa nguvu ya Mungu. Ili kupata neema hizo za Kimungu sisi tunahitajika kuwa watii kwa Maaskofu wetu. Kwa vile wao wanafundisha na kutuelekeza mambo ya Kimungu yenye kutupatia wokovu, basi, ni utii wetu ndio utakaotustahilisha wokovu.

Nyakati zetu hizi zimeshuhudia uwepo wa kondoo wakaidi wanaowapiga wachungaji wao. Wapo watu wenye bahati mbaya kubwa sana ambao wao kazi yao ni kuwakorofisha wachungaji na kugombana nao daima. Kondoo watundu na wakorofi ambao wamevaa sura ya shetani, anayewatuma kuwasumbua, kuwakaidi hadharani maaskofu na kuwaletea kila aina ya fujo, hao ni kikwazo kikubwa kwa injili.

Kuna kondoo wanaotaka kuwaongoza, kuwatawala na kuwabinafsisha wachungaji wao. Hawasikii wala kutii chochote, ila wanadai kusikilizwa tena kwa maandamano! Haifai, ni aibu, kanisa letu halipo hivyo. Utaratibu na utii wetu, vitatupeleka kwa Mungu.

Hati hii, Christus Dominus, imeainisha kwa kina na mapana juu ya sura, nafasi na wajibu wa Askofu katika Jimbo. Lakini kwa uhalisia wote, Askofu hawezi kufanya kazi kamilifu endapo kondoo hawapo tayari kuongozwa na kutoa ushirikiano stahiki. Hati hii inaelekeza kwamba ‘Mchungaji na Kondoo’ wawe na lengo Mmoja. Basi mpendwa msikilizaji, kama tulivyowahi kusema, familia ni shule ya utii. Ni usikivu na utii unaofundishwa katika familia ndio utatujenga kuwa kondoo watii ndani ya Kanisa.

Na sisi katika jumuiya yetu tukiona mwenzetu fulani ana utamaduni wa kugombanagombana na maaskofu au na viongozi wa kiroho, tumshauri tu kuwa Kanisa letu halina tabia hiyo. Hiyo ni tabia ya shetani peke yake. Tukiwa wasikivu na watiifu, sauti ya wachungaji wetu itatufikisha kwa baba, kwa sababu wanafanya kila wawezalo ili tufike mbinguni.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.