2014-12-20 08:12:55

Noeli 2014: Wafanyakazi wa Vatican kukutana na Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, ameamua kwa moyo mkuu kukutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Vatican pamoja na familia zao Jumatatu, tarehe 22 Desemba 2014. Hili ni tukio la kihistoria, kwa kukumbuka kwamba, si rahisi sana kwa wafanyakazi wa Vatican kuhudhuria katika matukio kama haya kwani mara nyingi Baba Mtakatifu anapokuwa na shughuli, wao pia wanachakarika kuhakikisha kwamba, mambo yanakwenda kama yalivyopangwa!

Kwa Mwaka huu, Baba Mtakatifu anataka kuzungumza nao, ili kuimarisha moyo wa upendo na mshikamano katika familia kwa kutambua sadaka na majitoleo yanayotolewa na wafanyakazi wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa. Tukio la kutakiana kheri na matashi mema kwa Kipindi cha Noeli, linakuja wakati ambapo Mama Kanisa anawahimiza wanafamilia kuendelea kutangaza Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu, ili kusaidia pia mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015.
All the contents on this site are copyrighted ©.