2014-12-20 15:35:36

Nafasi ya Bikira Maria katika historia ya ukombozi!


Katika maandalizi ya michezo kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Noeli, mtoto Silvia alipewa kucheza nafasi ya Mama Maria. Lakini kumbe moyoni mwake hakuwa amefurahishwa. Kadiri maandalizi ya mchezo kwa ajili ya sherehe za Krismasi zilivyokaribia, mwalimu wake aligundua shida fulani katika uso wa Silvia. Naye hakusita kumwuliza kulikoni. Naye bila kusita akasema, ningependa zaidi kucheza nafasi ya malaika kuliko ya Maria. Sijisikii kufanana na Maria Mama wa Mungu. Huyu mtoto aliona ni afadhali kushika na kucheza nafasi ya malaika kuliko kucheza nafasi ya Maria Mama wa Mungu.

Leo tunasikia sehemu ya maandiko matakatifu juu ya kupashwa habari Bikira Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Kwamba atamzaa Yesu, yaani, mkombozi wa wanadamu.

Tunaendelea na tafakari yetu ya majilio -kipindi cha kumbukumbu na matumaini. Tunakumbuka aliyofanya Mungu na kutumainia ujio wake kama alivyoahidi. Katika Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio – Tulikumbushwa tuwe macho, tukeshe. Kipindi cha majilio ni katekesi fupi ya ufahamau wa mpango wa Mungu wa ukombozi.

Bila kuamini tukio la kuzaliwa Bwana itakuwa vigumu kuishi imani inayotokana na matukio ya mpango huo. Siyo rahisi kuamini Yesu aliyepo bila kuutambua na kuukubali huo mpango mzima. Kwamba alizaliwa, akaishi kati yetu, akateswa, akafa, akazikwa, akafufuka na kupaa mbinguni. Kuukataa ukweli huu ni sawa na kusherekea kuzaliwa kwa mtu ambaye hajazaliwa. Itakuwa ni maigizo tu bila ukweli wowote.

Katika Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio - Kila mtu alialikwa aingie kucheza. Utamu wa ngoma ni kucheza, siyo kuangalia.. Mfano wa mpiga muziki Paganini ambaye baada ya kucheza muziki kwa muda mrefu aling’amua baadaye kuwa muziki unatoka moyoni na si kwenye chombo anachotumia kupiga muziki. Mfano wa Yohana mbatizaji unajibu wasiwasi wetu - yeye aliingia kuicheza ngoma.

Katika Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio – Yesu yuko wapi? Kumbe Yesu yuko kati yetu - Yoh 1,26 – Yohane akawajibu akisema mimi nabatiza kwa maji katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Yohani anaongea waziwazi juu ya uwepo wa Kristo kati yetu. Wajibu wetu sisi wakristo ni kuendelea kumshuhudia huyo Kristo.

Katika Jumapili hii ya nne ya kipindi cha Majilio – tunaona haja ya kuwa na unyenyekevu na usikivu ili kusikia vizuri Mungu anasema nini. Katika sauti zote ambazo Maria angeweza kusikia hapa duniani aliitegea sikio sauti ya Mungu na kwa kutii kwake ameokoka yeye, na sisi tumepata kumjua Mungu.

Mtu mmoja alifananisha safari ya majilio kama mtu anayesafiri na katika safari yake anaingia kwenye shimo refu. Kwa kawaida kama shimo ni refu na huko mbele kuna mwanga basi kinachoonekana kwa mbali ni kamwanga kadogo sana. Unapokaribia mwisho kabisa unaanza kuuona ukweli yaani mwanga wenyewe ambao mwanzoni ulikuwa kidogo. Mfano huu uko wazi kwenye masomo yetu ya leo.

Katika somo la kwanza - tunasikia habari ya maisha ya Waisraeli jangwani. Kila wanapokaribia kukata tamaa, Mwenyezi Mungu anafanya jambo kubwa kwao. Na hata baadaye katika mazingira yao mapya, mapambano yanaendelea. Halafu tunaona Daudi - analindwa na Mungu, anapata pumziko toka kwa Mungu, toka pande zote, na hali ya utulivu waliyoahidiwa Waisraeli siku waliyoingojea inapatikana – katika Kum 12:9 – Daudi sasa aweza kupumzika.

Mungu, anamfanya maarufu katika ulimwengu huu. Nyumba yake na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Hata hivyo pamoja na shida na matatizo yote ya Daudi, lakini ahadi ya Mungu inabaki palepale. Pamoja na giza lote, mwishoni kuna mwanga wa Mungu.

Injili ni ushuhuda wa utimilifu wa hiyo ahadi ya Mungu. Miaka hiyo mingi iliyopita inakamilika katika Maria. Huyu Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai anachukua nafasi ya Daudi baba yake na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Katika 1 Kor 15,25 tunasoma hivi; maana sharti amiliki yeye hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Na katika Isa. 7,14 tunasoma hivi; kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara, tazama bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume naye atamwita jina lake Imanueli. Fiat ya Maria, yaani nitendewe ulivyonena ni itikio la mwanadamu linalofanya hilo liwezekane leo. Unyenyekevu wake unamwokoa yeye na sisi pia.

Katika somo la pili - Rum. 16:25 – tunaalikwa tufurahi pamoja na Paulo mtume - sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo. Hii ni imani inayookoa, inayofufua inayotia uhai. Kwa kifupi katika somo hili tunaona kuwa Kristo anakamilisha ufunuo. Ni nini maana yake kwetu? Au tunadaiwa nini sisi? Tunadaiwa utii wa imani, na upendo unaotuwajibisha pamoja. Katika hilo tutapata uhuru wa kweli na ukombozi mkamilifu.

Yesu ndiye ufunuo wa hiyo siri. Tukiwa bado katika fumbo hilo tunakumbushwa haja ya kuendelea kusonga mbele kumwendea Bwana ili tukutane naye na azaliwe tena leo katika maisha yetu.

Katika jumapili hii, tumekaribia mno kuona waziwazi ahadi za Mungu kiasi kwamba tunamwona Bwana hapa mbele yetu. Tuangalie matayarisho mbalimbali tuliyofanya. Tayari tunasikia habari ya kupashwa habari Bikira Maria kuwa atakuwa mama Mungu na itikio lake na majukumu ya huyo Mungu ajaye atakuwa mfalme juu ya nyumba ya Yakobo milele na bila mwisho.

Makutano ya Maria na malaika ni alama ya imani hai. Imani ni zaidi ya kusoma kilichoandikwa au kusadikishwa tu. Ni makutano kati ya kinachoonekana na kisichoonekana.
Mt. Luis 1X wa Ufaransa, alikuwa akisaini hati za ofisi siyo kama Mfalme Luis IX, ila kama Luis wa Poissy. Alipoulizwa sababu ya kufanya hivyo alisema – Poissy ni mahali nilipobatizwa ila katika basilica la Rheims nilitawazwa mfalme. Aliendelea kusema, nafikiria zaidi mahali nilipobatizwa kuliko pale nilipotawazwa mfalme. Ni kitu kikubwa zaidi kuwa mtoto wa Mungu kuliko kujulikana kama mtawala. Ubatizo wangu ni pasi ya kuingia utukufu wa milele lakini ufalme wangu utapotea mara tu baada ya kifo.

Fumbo la Kristo linaokoa. Tuwajibishwe na ushuhuda huu ili tuweze kuishi vizuri zaidi imani yetu. Mtakatifu Agustino anasema Maria aliyejaa neema alimchukua Yesu katika moyo wake kabla ya kumchukua tumboni. Hakika sisi hatuwezi kumzaa mwokozi. Kwanza tayari keshazaliwa. Twaweza kumwonesha hapa ulimwenguni kwa kuwa watu wake Mungu. Mungu atuita kwanza kama Maria, halafu hutupatia utume fulani wa kufanya. Tukijibu wito huo, twamwonesha Mungu hapa duniani. Ndilo jibu kubwa na la pekee tuwezalo kumrudishia Mungu na watu wake tunaposherehekea sikuku ya Noeli mwaka huu na wakati wote.

Angalia alichofanya Daudi kujenga ufalme, halafu anatambua kuwa hajafanya mengi kwa ajili ya Mungu. Anataka kumjengea nyumba Mungu. Katika somo la kwanza tunaona nabii Nathan anamwangalisha mfalme Daudi kuwa si yeye atakayejenga nyumba ya Bwana, yaani hekalu, bali ni Mungu mwenyewe atakayemjengea Daudi nyumba. Aidha Mungu anatambua mawazo na nia yake na anajenga yeye nyumba ya ufalme wake.

Aidha tunatambua kuwa Mungu hahitaji nyumba ya kujengwa na mawe. Yeye ahitaji kupokelewa nasi na kumshuhudia hapa ulimwenguni. Jambo zuri zaidi katika ahadi hiyo ya Mungu ni kwamba huo ufalme mpya utatawala milele. Maagizo haya yanadokeza kuwa katika kizazi chake atazaliwa mtoto wa pekee atakayependekezwa na Mungu. Uchaguzi huu ni wa kwanza katika mfululizo wa maagizo juu ya masiya mwana wa Daudi - Isa: 7:14, Mik. 5,1, Hag 2,3 na katika Agano Jipya – Mdo: 2,30 yanaeleza uchaguzi huu kuwa ni Kristo.

Kwa mfano katika Mt. 12: 46-50 tunasoma habari juu ya jamaa za kweli za Yesu. Jibu la Yesu litusaidie pia kutafakari mwito wa Yesu kwetu sisi. Yesu ategemea wafuasi wake wawe si tu kaka na dada, bali wale wanaomshuhudia yeye na kushika Neno lake. Mama yake pia katika Lk. 1,38 – anasema, tazama mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema, kisha malaika akaondoka akaenda zake. Hili jibu la Maria ni zuri sana na linatupa changamoto sote kuwa tayari kutimiza mapenzi ya Mungu.

Angalia alichofanya Maria - mimi ni mtumishi wa Bwana. Ujio wa Kristo ni ushindi dhidi ya ulimwengu geugeu. Msimamo wa Mama Maria unaleta ukombozi kwa ulimwengu, pamoja na Maria twaweza kuimba sifa ya Mungu - moyo wangu wamtukuza Bwana na roho yangu inafurahi katika Mungu mwokozi wangu. Yeye daima aliendelea kukua katika imani.

Tumsifu Yesu Kristo.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.