2014-12-20 08:03:01

Mshikamano dhidi ya baa la njaa duniani!


Baa la njaa bado ni janga kubwa la kimataifa linaloendelea kufyeka maisha ya watu zaidi ya millioni mia nane na tano kadiri ya taarifa zilizotolewa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, kati yao kuna watoto millioni tatu wenye umri chini ya miaka mitano wanaoteseka kutoka na utapiamlo wa kutisha. Baa la njaa, ugonjwa wa Ukimwi, Malaria na Kifua kikuu ni chanzo cha vifo vya maelfu ya watu duniani kila mwaka.

Kwa kuguswa na mahangaiko ya watu wengi duniani, Kamati ya Kanisa Katoliki nchini Ufaransa ya mshikamano wa maendeleo na dhidi ya baa la njaa, Ccfd, katika kipindi cha Majilio, linaendesha kampeni ya kuchangia kwa hali na mali dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha: Barani Afrika, Amerika ya Kusini, Asia na Mashariki ya Kati.

Hii ni kampeni ambayo inaungwa mkono na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, ili kuwahamasisha waamini na wananchi wenye mapenzi mema kulivalia njuga baa la njaa duniani, kwa kutambua kwamba, binadamu wote wanaunda Familia moja ya Mungu. Watu wanaoteseka kwa baa la njaa wasaidie kuamsha dhamiri nyofu, ili kwa pamoja, watu waweze kuunganisha nguvu zao dhidi ya baa la njaa na utapiamlo ambalo kwa sasa ni janga la kimataifa.

Lengo la kampeni hii ni kusaidia mchakato wa kuwajengea wananchi uwezo wa kupambana na baa la njaa kwa kuboresha uzalishaji, utunzaji na ugavi wa mazao ya chakula. Kampeni hii kwa namna ya pekee, inawaalika kuguswa na mahitaji ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na baa la njaa duniani.

Ni changamoto pia ya kupambana na mambo ambayo yanaendelea kusababisha baa la njaa na umaskini duniani, kutokana na ufisadi; ubinafsi; matumizi ya uoto nishati; ukwapuaji wa maeneo makubwa ya ardhi kutoka kwa wakulima wadogo wadogo kwa kisingizio cha uwekezaji mkubwa. Kampeni dhidi ya baa la njaa na utapiamlo inaendeshwa kwa kutumia vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.