2014-12-20 15:12:51

Maskini ni hazina kubwa kwa Kanisa na binadamu katika ujumla wake!


Shirikisho la Jumuiya ya Yohane XXIII linatekeleza utume wake katika nchi 34 duniani na Barani Afrika wako: Zambia, Tanzania, Kenya, Burundi na Cameroon. Ni shirikisho linalowajumuisha Wakleri, Watawa na Waamini Walei, ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwani linatambuliwa na Mama Kanisa katika jitihada za kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Shirikisho hili lilianzishwa na Padre Oreste Benzi, ambaye hivi karibuni Jimbo Katoliki la Rimini Italia, limeanzisha mchakato, ili aweze kuandikwa katika orodha ya majina ya Wenyeheri ndani ya Kanisa, kwani anatambulikana sana kutokana na mchango wake wa huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kama ambavyo aliwahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.

Ni Shirikisho linalojibidisha kuwaendea na kuwahudumia maskini na wahitaji zaidi, kwa kuwarudishia utu na heshima yao wanawake na wasichana waliokuwa wametumbukizwa katika utumwa mamboleo pamoja na kuwahudumia maskini wanaojionesha kwa sura na kwa nyakati tofauti.

Huu ni ushuhuda uliotolewa na Bwana Giovanni Paolo Ramonda, Mratibu mkuu wa Shirikisho la Jumuiya ya Yohane XXIII walipokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican siku ya Jumamosi, tarehe 20 Desemba 2014. Anasema, kuna idadi kubwa ya vijana wanaotaka kukutana na Yesu katika umaskini na utupu wao; kuna maelfu ya watu wanataka pia kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo; kwa hakika kuna watu wanaotaka kukutana na Yesu kwa njia ya Kanisa linalowajali na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Shirikisho hili linapenda kuendelea kubeba Msalaba kwa kusaidiana na maskini, kwa kuwashirikisha nguvu inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na matendo ya huruma, kwa kutambua kwamba, maskini na wanyonge ni hazina kubwa kwa Kanisa na binadamu katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio vaticanAll the contents on this site are copyrighted ©.