2014-12-20 15:12:54

Mama ana kila sababu ya kuheshimiwa.


Katika wakati huu, ambamo tunaekea kilele cha sikukuu ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, Makala "Dunia Mama" kwa mara ingine, anawakaribisha kutafakari pamoja, heshima na wito wa mwanamke kama mama. Nani kama Mama....ingawa mikono yake ni midogo na nyororo, huduma yake ni kubwa na yenye nguvu za ajabu!i

Mwanamke ameumbwa na asili ya kupenda.Huwapenda viumbe na kuvihudumia, kama tunavyoona katika maisha yakila siku. Kwa mwanamke, kazi na huduma ni pete na chanda, kama ilivyokwisha thibitishwa kisayansi pia kwamba, kuna tofauti kubwa katika hulka na hisia asilia, kati ya mwanamke na mwanamme. Mwanamke kaumbwa na asili ya upendo wa kipekee katika kuhudumia binadamu wengine. Mwanamke hutimiza wajibu huu, huhudumia kwa furaha, hufurahia kubeba mimba kwa muda wa miezi tisa tumboni mwake matumaini, akivumilia hali zote za masumbufu na kujinyima kwingi, akiwa amejawa na upendo na matumaini mapya, ya kuongeza binadamu mwingine duniani. Ni maumbile ya ajabu aliyoumbwa nayo mwanamke. Maumbile yaliyojaa upendo asili.

Na ndiyo maana, hushangaza sana pale linaposikika tukio la Mama kumuua mtoto wake. Hata hivyo, ukichimba kwa ndani kiini cha matukio mengi ya aina hiyo, utaona kwamba, ukatili huo ulilenga kusahihisha tabia ya mtoto husika, mtoto aliye onekana kuwa na tabia sugu isiyompendeza mama katika mambo fulani fulani. Mfano Mama kumchoma kwa moto mikono ya mtoto wake kwa sababu mtoto kaiba nyama chunguni, au kadokoa mlo kabla ya wengine. Adhabu hiyo ya mama kwa mara nyingi hulenga zaidi katika kurekebisha tabia ya mwanae , asije kuwa mwizi, au pengine mtoto kutokuwa sikivu katika kufuata masharti na kanuni za kijamii. Kweli adhabu kama hizo, hazifai,ni upendo unaopita kiasi, katika kurekebisha kasoro.
Vitabu na Maandiko Matakatifu ya Kanisa , tangu agano la kale, agano Jipya na nyaraka mbalimbali za Kitume za Mapapa na Kanisa, mna maelezo ya kutosha juu ya heshima na wito wa mwanamke katika kuwa Mama. Vyote huonyesha waziwazi juu ya heshima ya mwanamke katika maisha ya binadamu na pia katika mpango wa wokovu wa Mungu kwa binadamu. Tunasoma katika Kitabu cha Isaya juu ya utabiri wa kuzaliwa kwa Mkombozi na mwanamke “Tazama Bikira atachukua Mimba atazaa mtoto mwanamme naye atamwita jina lake Emanueli” Is 7:14. Vivyo hivyo imeandikwa katika Injili ya Matayo habari hii ya Mkombozi wa dunia kuzaliwa na mwanamke , Mama Bikira Maria (tz Mt 1:22-23)”. Binti Mtukufu wa Sayuni aliye bora sana Mkingiwa dhambi ya asili , nyakati zilipotimia kwa mpango wa wokovu kutimizwa , Mwana wa Mungu alitwaa maumbile ya binadamu ili amkomboe binadamu katika dhambi zake kwa fumbo la mwili wake.

Vivyo hivyo mafundisho ya Kanisa , kama ilivyoainishwa katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, yatuonyesha waziwazi juu ya huruma ya Mungu kwa binadamu, iliyotufanikisha pia kuitwa wana wa Mungu, kupitia Mpango wake mtimilifu wa kumwilisha mwanae pekee, nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu Yesu Kristo, ndani ya tumbo la Mwanamke , aliyeteuliwa tangu milele, awe mama ili kwamba , kama vile mwanamke alivyoshiriki katika mauti , kadhalika mwanamke asaidie kuuleta uzima. Kwa namna ya pekee Mama wa Yesu anauzalia ulimwengu uzima wenyewe , yeye atengenezaye yote upya , naye alitajirishwa na Mungu, karama za kustahili jukumu hili kubwa la kumzaa mwana wa Mungu. Mwanamke anapata heshima hii katika asili yake ya kuwa na upendo wa kuhudumu wengine. Mwanamke anakuwa katika kiini cha tukio hili la wokovu kwa binadamu.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unasema, Mungu kwa namna ya kipekee alimshirikisha mwanamke katika siri hii ya uumbaji wa maisha , ndani ya tumbo la mwanamke. Mwanamke mja mzito, anapata kujazwa na furaha ya ajabu ya maisha haya mapya yanayokua polepole ndani mwake, na kwa hisi za kipekee huendelea kutambua kinachoendelea ndani yake. Katika mwanga wa "mwanzo wa maisha ", mama anapokea na kukipenda kama mtu, kiumbe kilicho ndani ya tumbo lake .
Baba Mtakatifu Yohana Paulo II katika waraka wake wa Hadhi ya Mwanamke,”Mulieris Dignitatem” akitazama kwa makini utume wa wanawake katika Injili, aliandika kwamba, kwa mara nyingi wanawake waliokutana au kuandamana na Yesu katika safari zake za kutangaza Habari njema ya wokovu mijini na vijijini , walipata neema nyingi kutoka kwake. Yesu aliwataja wanawake kama mfano katika kuupata ukweli juu ya ufalme wa Mungu. Tuna mifano ya sarafu iliyopotea ( Lk 15: 8-10), mfano wa chachu (Mt 13:33), mfano wa wasichana wenye busara na wapumbavu (Mat 25: 1-13), mwanamke mjane , aliyetia sarafu mbili za shaba katika sanduku la sadaka n.k. Katika mifano hiyo, Yesu anaonyesha heshima zake kwa wanawake hawa, kama mfano wa kuigwa na kila mtu mwenye kuwa na imani. Na pia Yesu anaonyesha utetezi kwa wanawake, wanaogandamizwa na mifumo ya kijamii na kisheria (Lk 18: 1-7).

Mtakatifu Yohana Paulo 11 anaendelea kusema, katika mafundisho yote ya Yesu , tunaona kwamba, kamwe Yesu hakuwa na ubaguzi dhidi ya wanawake. Kinyume chake, maneno yake na kazi zake daima huonyesha heshima na sifa kwa wanawake. Wakati Yesu akitembea katika njia yake ya Mateso kuelekea Golgotha, aliwageukia wanawake na kuwaambia, “enyi binti wa Yerusalemu , msinililie mimi”, (Lk 23:28). Yesu anaonyesha huruma yake kwa wanawake, hata wale waliokuwa wametenda dhambi , hakuwadharau au kuwabeza, lakini kwa upole na unyenyekevu aliwataka wageuze maisha yao.

Mpendwa, kuna matukio mengi tu yaliyotajwa katika Injili , ambamo tunaona wanawake wengi, wa umri tofauti, maisha tofauti , wagonjwa, au mateso kimwili, waliokutana na Yesu, kama yule mwanamke aliyegusa vazi la Yesu, au mama mkwe wa Simon , ambaye " alikuwa na homa amelala kitandani ana homa kali, binti wa Yairo, mwanamke Mjane , mwanamke Mkanaani na kadhalika. Matukio yote haya yanatuonyesha kwamba, imani na unyenyekevu na upendo na ukuu wa roho aliyo nayo mwanamke hata katika safari ya maisha ya kiroho. Yesu alimwambia mwanamke Mkanani , aliyemwita Yesu Unirehemu Bwana , binti yangu amepagwa sana na pepo, Yesu alimjibu, Mama , imani yako ni kubwa , na iwe kwako kama utakavyo (Mt 15:28).

Katika mwanga wa Injili , tunaona kwamba, mwanamke ameinuliwa , si tu kimwili lakini kwa kila asikilizaye Neno la Mungu na kulishika , anapata hadhi ya kuitwa pia mwana wa Mungu. Kwa hiyo historia ya binadamu, kupitia uzao wa mwanamke , daima inakuwa na uhusiano na Mkataba na Mungu, kwa njia ya Mama wa Mungu.

Katika Injili ya Yohane 1: 12 imeandikwa , bali wote walio mpokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu , ndio wale waliaminio jina lake, waliozaliwa si kwa damu wala si kwa mapenzi ya mwili wala mapenzi ya Mtu, bali kwa Mungu. Na pia katika waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi, ameandikwa, historia ya kila mwanadamu inapitia katika nguzo hii ya mwanamke, kwenye siri ya kuitwa watoto wa Mungu (Rum 8: 19).

Kwa maelezo hayo, Dunia Mama anatoa mwaliko , kwetu sote, tutazame maisha yetu ya kawaida mahali popote tulipo, tulinganishe mahangaiko ya kuhudumia ndani ya familia, kati ya baba na mama . Ukweli ni kwamba Mama daima hutumia muda wake kuihudumia familia katika mambo ya kawaida madogomadogo lakini msingi sana katika maisha ya kawaida ya familia. Utaona ni kweli mwanamke kazaliwa na upendo wa ajabu katika kuhudumia wengine. Tazama jinsi anavyo hangaika kuhakikisha familia inapata mlo wake wa kila siku tena kwa wakati waliouzoea. Tazama jinsi mama anahudumia watoto na wagonjwa. Tazama jinsi wanavyowainamia wasiojiweza, na kuwapa kila msaada wanaohitaji? Mikono yake midogo na laini, muda wote ikijishughulisha na utoaji wa huduma, na zaidi huwa wakati wa madhimisho ya Siku Kuu kana hii ya ya Noel , anahangaika huko na kule, walau siku hiyo, mazingira ya familia yapendeze, watoto wavae vizuri , wapate mlo tofauti na siku zote,angalau pilau na chapati zisikosekane.

Mpendwa ,tafakari yetu haina maana ya kusahau ukarimu na wema wa Baba, lakini basi ni mwaliko wa kutathimini kwa makini heshima ya Mwanamke ndani ya Familia, kama ufunguo wa maisha bora. Dunia Mama leo hii, inawasihi nyote katika Siku Kuu hii ya Noel, tunapo mpongeza Mama Maria kwa kutuzalia Mtoto Yesu, Mkombozi wetu , basi pia tusisahau kununua zawadi hata kama ni dogo tu , kwa ajili ya kumpongeza mama nyumbani , kwa huduma yake ya kila siku, inayotuwezesha kusonga mbele na Maisha. Jamani nani Kama Mama! Tumheshimu na kumpa upendo wote kwani ni mastahili yake.
All the contents on this site are copyrighted ©.