2014-12-20 15:07:50

Kweli kuna watu wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi wa jirani zao!


Shirikisho la Jumuiya ya Yohane wa XXIII ni ushuhuda unaoonesha uwepo wa utumwa mamboleo na ubinafsi kiasi cha kuwageuza baadhi ya watu kuwa kama bidhaa na kwa upande mwingine kuna kundi la watu linaloendelea kujisadaka kwa kuwaonjesha waathirika wa biashara hii upendo na kuwainua tena kimaisha na kimaadili.

Hiki ni kielelezo tosha kabisa cha sura mbali mbali za umaskini ambazo zinaendelea kusababisha madonda makubwa katika ulimwengu, lakini mbaya zaidi ni tabia ya ukanimungu, unaomwondoa Mwenyezi Mungu katika maisha ya mwanadamu na badala yake, uchu wa mali na fedha vinapewa kipaumbele cha kwanza.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana, akasikiliza shuhuda mbali mbali na hatimaye akazungumza na wanachama wa Shirikisho la Jumuiya ya Yohane XXIII. Baba Mtakatifu anasema, uwepo wa Mwenyezi Mungu unaweka mambo bayana kati ya uhuru na wema; kati ya utumwa na ubaya na kati ya watu ambao wanaweza kuwasaidia jirani zao kwa njia ya matendo mema kuonja tena ile furaha inayobubujika kutoka moyoni.

Ni uwepo endelevu unaopanuka na kuenea; unaosafisha na kutakasa mawazo na hisia za watu na hatimaye, kuwapatia watu nguvu inayohitajika katika kukabiliana na magumu ya maisha. Pale ambapo Yesu amepewa kipaumbele cha kwanza kuna ufufuko, maisha mapya kwani Yesu ni ufufuko na uzima, kielelezo cha imani tendaji inayojali na kuguswa na mahangaiko ya watu, kwa kufuata mfano wa Msamaria mwema.

Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Padre Oreste Benzi, mwanzilishi wa Shirikisho hili, aliyekuwa na upendo wa pekee kwa maskini, watoto, watu waliokuwa wametengwa na kung'olewa kutoka kwenye upendo wa Kristo Mteswa, aliyejinyenyekesha na kuwa maskini kwa ajili ya maskini; upendo unaojionesha kati ya watu wa mataifa, wanaoendelea kushirikishwa imani kutoka kwa Kristo Mfufuka anayetekeleza utume wake kwa njia ya Wasamaria wema, kwa kutumia rasilimali kidogo iliyopo ili kuwaonjesha watu upendo na huruma ya Mungu, kama alivyofanya Yesu kwa kuwalisha maelfu ya watu kwa mikate mitano na samaki wawili.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni utume wa ajabu ulioanzishwa na Padre Oreste Benzi, akawa na ujasiri wa kuwakutanisha watu na Kristo ili kukutana na Yesu kama: Shujaa na rafiki kwa njia ya shuhuda za maisha yanayobubujika kutoka katika Ukristo. Jumuiya hii leo hii inatekeleza utume wake katika nchi 34, zikiwa na nyumba za familia, vyama vya ushirika, elimu, nyumba za sala pamoja na mahali pa kuwahudumia wanawake wajawazito. Neema na baraka ya Mwenyezi Mungu imewawezesha wanachama wa chama hiki kukua na kuendeleza karama ya mwanzilishi wao, aliyekazia umuhimu wa sala.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka wanachama hawa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika majiundo endelevu, kwa kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kisakramenti, hasa zaidi kwa kupokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na kuwasaidia watu katika medani mbali mbali za maisha, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.