2014-12-20 08:36:31

Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, linapendeza!


Viongozi waaandamizi kutoka Vatican pamoja na watu wenye mapenzi mema, Ijumaa jioni tarehe 19 Desemba 2014 wameshuhudia sherehe za uzinduzi wa mfumo mpya wa umeme kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican unaolenga kuboresha mandhari ya Kanisa kuu pamoja na kuendelea kubana matumizi kwa kuwa na muda wa miaka kumi kabla ya kuanza kufanyia matengenezo makubwa. Huu ni mchango mkubwa uliotolewa na kampuni ya umeme ya Italia, ACEA pamoja na wadau wengine.

Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anasema, maboresho ya mfumo wa umeme kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Siku kuu ya Noeli, ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kufanya tafakari ya kina kuhusu Yesu Kristo, Mwanga wa Mataifa anayekuja kufukuza giza katika mioyo ya watu, ili waweze kutembea tena katika mwanga wa Kristo.

Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anasema Kardinali Comastri, lina umuhimu wa pekee sana katika maisha na utume wa Kanisa, kwani hapa ni mahali ambapo Mtakatifu Petro aliyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; hadi leo hii, Kanisa linaendeleza dhamana na utume ambao Yesu alimkabidhi Mtakatifu Petro ambaye kimsingi ni mwamba wa Kanisa.

Kardinali Angelo Comastri ametumia fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru wafanyakazi wote wa ACEA waliojitosa kimasomaso ili kuhakikisha kwamba, zoezi hili linafanikiwa kwa kuzingatia ubora na viwango vya kimataifa na kwa muda uliopangwa. Kazi ya mafundi umeme inayoonesha weledi mkubwa, itaendelea kukumbukwa na watu wengi!







All the contents on this site are copyrighted ©.