2014-12-20 09:02:42

Hija ya Papa Francisko nchini Sri Lanka ni neema na baraka!


Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka linasema linaendelea kukamilisha maandalizi kwa ajili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Januari 2015. Waamini wanataka kumwonesha Khalifa wa Mtakatifu Petro umoja, upendo na mshikamano, kwa kumshukuru Mungu kwa zawadi na baraka kuu ya ujio wa Baba Mtakatifu nchini Sri Lanka.

Lengo la hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Sri Lanka, kwanza kabisa ni kutaka kuwaimarisha ndugu zake katika imani, mapendo na matumaini, kwa kuendelea kujikita katika utangazaji na ushuhuda wa amani unaofumbatwa katika ukweli, uwazi na upatanisho. Lengo la pili ni kumtangaza Mwenyeheri Joseph Vaz kuwa Mtakatifu, ndiyo maana hija ya Baba Mtakatifu nchini humo inatarajiwa kuwa ni cheche za matumaini kwa Kanisa na kwa watu wote wenye mapenzi mema.

Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka linaitaka Serikali na wanasiasa kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo tarehe 8 Januri 2015, unakuwa ni huru, haki na wa amani, ili kutoa fursa ya matumaini ya Sri Lanka iliyo bora zaidi kwa siku za usoni. Mchakato wa upigaji wa kura, umepunguza makali ya maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Sri Lanka, lakini yote haya ni mapenzi ya Mungu wanasema Maaskofu.

Kanisa litaendelea kukazia umuhimu kwa waamini na Jamii katika ujumla wake, kujikita katika uaminifu, ukweli na haki, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kama ambavyo Yesu mwenyewe anawataka wafuasi wake kufikiri na kutenda. Ni changamoto ya kuwa ni sauti ya wanyonge ndani ya jamii, ili kujenga na kudumisha amani ya kudumu kati ya watu.

Maaskofu wanasema, uchaguzi mkuu nchini Sri Lanka upanie kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa na kamwe uchaguzi usitumiwe kuwa ni uwanja wa fujo na patashika nguo kuchanika; huku haki, aman, ustawi na maendeleo ya wengi yakipewa msukumo wa pekee. Maaskofu wanawashukuru wananchi kwa kuonesha ukomavu pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuwaunga mkono katika mchakato wa kujipatia maendeleo endelevu.All the contents on this site are copyrighted ©.