2014-12-19 07:56:26

Wahudumieni wananchi kwa kuzingatia: ukweli, uwazi na uaminifu!


Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika mahubiri yake kwa Wabunge wa Italia, kama sehemu ya maadhimisho ya maandalizi ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2014, amewataka Wabunge na viongozi wa Serikali katika ujumla wao, kuhakikisha kwamba, wanawahudumia wananchi kwa kutumia: ujuzi, maarifana weledi; mambo yanayojikita katika: uaminifu, nidhamu, ukweli, uwazi na majitoleo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Wanasiasa wanapaswa kukumbuka kwamba, wamepewa dhamana na wananchi kwa ajili ya kusaidia mchakato wa kuwaletea maendeleo na wala si fursa ya wanasiasa hawa kujitajirisha au kutafuta mafao binafsi, mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha lengo la wananchi kuwapatia dhamana ya kuwaongoza!

Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa pia na viongozi wakuu wa Bunge na Serikali ya Italia. Kardinali Bagnasco anasema, Fumbo la Umwilisho wa Mwana wa Mungu ni changamoto kwa viongozi waliopewa dhamana na wananchi kuwa kati ya wananchi ili kuwahudumia kwa hekima na busara; huku wakisimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Fumbo la Umwilisho, liwasaidie kujikita katika kutafuta, kuufahamu na kuukumbatia ukweli, ili haki, amani na ustawi wa wengi viweze kushika mkondo wake. Haya ndiyo malengo makuu ya mchakato wa uongozi katika siasa! Wanasiasa wakumbuke kwamba, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu na kwamba, hii ni fursa makini kwa mtu kuweza kujiendeleza mwenyewe na familia yake.

Mwanadamu anapokosa fursa za ajira, anajisikia mpweke na utu wake kuanza kuingia mashakani. Wanasiasa wawe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, wanatunga sera makini zitakazowawezesha watu kupata ajira pamoja na kuendelea kuwa na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya. Maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, ni wakati muafaka wa kutakiana kheri na fanaka; ukweli na uwazi; sadaka na majitoleo, ili kushinda cheche za maovu zinazotaka kupenyeza miongoni mwa watu kwa kujikita katika uchu wa mali. Kila raia anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.