2014-12-19 10:37:13

Caritas Mbeya yapongezwa kwa kufanikisha utoaji wa huduma!


Mkurugenzi wa Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania, Edgar Mangasila amewapongeza wafanyakazi wote wa Idara hiyo kwa kushirikiana kwa pamoja katika kufanikisha adhma ya Idara hiyo katika utume kwa jamii kwa ari na kasi.

Akizungumza katika kikao cha wafanyakazi wote kilichofanyika Ijumaa, tarehe 19 Desemba 2014 lengo likiwa ni kufunga ofisi kwa ajili ya mapumziko ya siku kuu ya Noel ikiwemo nafasi ya kujitathmini kwa mwaka mzima katika utume wa Idara hiyo, Mangasila amesema, wakati tunaelekea kufunga mwaka ni vema kujitathmini na kujipanga upya mwaka ujao.

Mkurugenzi huyo amesema, watumishi tunapaswa kujipongeza kwa kufikia malengo ya utume wa Caritas katika jamii na kwamba pongezi hizo ziwaendee na wenzi wao ambao kwa namna moja ama nyingine wamesaidia kufanikisha malengo hayo. "Hata hivyo niwasihi sana tujipange upya kwa mwaka 2015 katika utume wetu...upande wa nidhamu nawashukuru mnafuata maadili mema kadiri Mwenyezi Mungu anavyotuongoza katika maeneo yote katika makazi tunayoishi na maeneo ya kazi,"amesema.

Ameongeza,"Sisi ni watumishi wa watu na sote tupo kwa ajili ya watu na tuendelee kudumisha ushirikiano kama tulivyoonesha mwaka huu na tujitume zaidi,ili jamii yenye wahitaji iendelee kunufaika zaidi."

Ni utamaduni wa Idara ya Caritas Jimbo Katoliki la Mbeya kwa idhini ya Mhashamu Baba Askofu Evaristus Marcus Chengula (IMC) wa Jimbo Katoliki la Mbeya watumishi kupumzika kwa ajili ya kusherehekea Siku kuu ya NOeli na Mwaka Mpya ikiwemo nafasi ya kujitafakari na kujipanga upya kwa ajili ya utume wa Kanisa katika jamii.

Hata hivyo Mkurugenzi Mangasila amesema licha ya kupumzika watumishi wasijisahau katika utume wao wa kila siku katika familia na Kanisa; utume ambao haupumziki moja kwa moja kwani pale wanapohitajika wanapaswa kuwa wepesi na kuitikia wito mara moja kwa kutoa huduma hitajika haraka iwezekanavyo.

Na Thompson Mpanji, Mbeya. Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.