Amani inayopaswa kutawala katika mioyo ya watu ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu
inayoambatana na: upendo, furaha, uvumilivu, utu wema, uaminifu, upole, kiasi, juu
ya mambo kama hayo hakuna sheria anasema Mtakatifu Paulo na kwamba, kuna tofauti ya
karama, changamoto na mwaliko kwa waamini kushirikiana na neema ya Roho Mtakatifu
katika uhuru kamili. Amani kama zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu inajionesha katika
utulivu wa moyo na hii ndiyo ambayo watu wengi wanayohitaji katika maisha yao.
Amani
ya ndani ni kati ya mambo ambayo Mama Kanisa amependa kuyaendeleza katika historia
ya maisha ya mwanadamu na tasaufi ya Kanisa, iliyokuzwa na kupanuliwa zaidi na Mtakatifu
Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, kwani moyo wa mwanadamu hauwezi kutulia wala
kupata amani ya kweli hadi pale utakapoungana na Muumba wake, kwa kutekeleza mapenzi
yake na hatimaye, kupata amani ya milele.
Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa
na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri mkuu wa Nyumba ya Kipapa, kama sehemu ya maadhimisho
ya Kipindi cha Majilio, mahubiri ambayo yametolewa Ijumaa tarehe 19 Desemba 2014 kwenye
Kikanisa cha Mama wa Mkombozi, mjini Vatican. Anasema, njia ya amani ni kanuni msingi
ya mang'amuzi katika maisha ya mwanadamu mintarafu mapenzi ya Mungu kwa kuhakikisha
kwamba, mapambano ya maisha ya kiroho dhidi ya mapungufu ya kibinadamu yanakuzwa na
kuendelezwa zaidi. Ni changamoto na mwaliko wa kubeba vyema Msalaba na kuanza kumfuasa
Yesu katika njia ya Msalaba na kuishi kadiri ya mang'amuzi ya maisha ya kiroho.
Amani
ya ndani ni sehemu ya mchakato wa nguvu inayooneshwa na mwamini kwa kushirikiana na
Roho Mtakatifu, kwa kusikiliza kwa makini na kumwilisha Mafundisho ya Roho Mtakatifu
katika uhalisia wa maisha, katika hali ya unyenyekevu. Mwamini anayetekeleza mambo
haya katika maisha yake anaweza kuingia katika ufalme wa amani na utulivu wa ndani,
daima akijitahidi kumfuasa Kristo.
Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi
Mungu yuko tayari kumlinda na kumtegemeza mtu ambaye anategemea na kumwaminia katika
amani kamilifu; ndiyo changamoto inayotolewa na Yesu kwa wafuasi wake kutojitaabisha
mno na kesho ambayo tayari iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto kwa
waamini kujenga matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwamba salama.
Wakati
huu, waamini wanapojiandaa kuadhimisha Siku kuu ya Noeli wanapaswa kutunza amani ndani
mwao kwa kutambua kwamba, wanapendwa na Mwenyezi Mungu na zawadi ya kwanza ambayo
mwanadamu amepewa katika Fumbo la Umwilisho ni amani duniani kwa watu wanaopendwa
na Mwenyezi Mungu na hii ni zawadi kwa wote pasi na ubaguzi.
Je, ni nani anayeweza
kuwatenga watu na upendo wa Mungu anauliza Mtakatifu Paulo, Je, ni dhiki, shida, adha,
njaa, utupu, hatari au upanga? Haya ni mambo ambayo yanaleta shida na mahangaiko katika
maisha ya mwanadamu, lakini hakuna kitu kinachoweza kuwatenga na upendo wa Mungu ulio
katika Yesu Kristo. Licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, mwanadamu bado anaendelea
kubaki kuwa ni dhaifu kutokana na uwepo wa magonjwa yasiokuwa na tiba na vitendo vya
kigaidi; yote haya yanapita, lakini mtu ambaye amejikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu
hawezi kupungukiwa na chochote. Noeli iwe ni kipindi cha amani inayojikita kwa Mwenyezi
Mungu, jirani na katika moyo wa mtu binafsi!.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.