2014-12-18 07:24:03

Zambia na watu wake!


Askofu mkuu Ignatius Chama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia anasema kwamba, katika kipindi cha miaka 50 tangu Zambia ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingereza, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika nyanja mbali mbali za maisha, ingawa utandawazi bado unaendelea kuwatumbukiza Wazambia wengi katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato. RealAudioMP3

Zambia imebahatika kuwa na rasilimali nyingi, lakini bado hazijatumika kikamilifu kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Zambia. Ugonjwa wa Ukimwi ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya familia nyingi, kwani athari zake ni kubwa kwa familia na jamii katika ujumla wake.

Askofu mkuu Chama anasema, wananchi wa Zambia kwa sasa wako kwenye mchakato wa kampeni kwa ajili ya kumpata Rais atakayemrithi, Marehemu Michael Chilufya Sata alifariki dunia hivi karibuni, akiwa anapata matibabu nchini Uingereza. Lakini ikumbukwe kwamba, kunako mwaka 2008 Zambia ilimpoteza pia Rais Levy Mwanawasa, wakati alipokuwa anahudhuria mkutanio wa Umoja wa Afrika.

Katika kipindi cha siku tisini, kadiri ya Katiba, wananchi wanapaswa kufanya uchaguzi, ndiyo maana kwa sasa Zambia ni patashika nguo kuchanika, kila Rais mtarajiwa anaendelea kujinadi kwa Chama chake ili aweze kupewa nafasi ya kupeperusha bendera wakati wa uchaguzi mkuu.

Zambia katika uwanja wa kisiasa inaendelea kupita katika kipindi kigumu sana ingawa hawajafikia hatua ya baadhi ya watu kuingia mstituni ili kuendesha mapambano ya silaha. Wananchi wamefikia kiwango kikubwa cha ukomavu katika masuala ya kisiasa, lakini bado wanahitaji kuendelea kukua na kukomaa zaidi, ili kutafuta mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Ili kufikia ukomavu wa kisiasa kuna haja ya watu kuendelea kujifunza na kupima mafanikio yao kwa hekima na busara zaidi.

Kanisa nchini Zambia kwa asili ni la Kimissionari, lakini nalo pia linaendelea kukomaa kwani sehemu kubwa ya mihimili ya Uinjilishaji ni Wazambia wenywe, jambo linaloonesha ukomavu katika kujitegemea na kulitegemeza Kanisa katika rasilimali watu. Kanisa Katoliki nchini Zambia linaendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu kwa njia ya watawa mbali mbali wanaofanya kazi ndani na nje ya Zambia na Afrika katika ujumla wake. Umissionari ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki nchini Zambia.

Takwimu zinaonesha kwamba, Kanisa Katoliki Zambia limewekeza sana katika sekta ya elimu, utume ulioanza kunako mwaka 1895 kwa kuanzisha shule za awali, sekondari na vyuo vya ufundi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linashiriki kikamilifu katika majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa kumpatia elimu bora, itakayomwezesha kupambana na mazingira, ili Zambia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Kanisa limewekeza sana katika sekta ya afya, kiasi cha kujenga mtandao wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, huduma inayoratibiwa na Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika sekta ya afya. Zambia ina hospitali 18 na Zahanati 38 na kwamba, asilimi 60% ya vituo vyote vya afya nchini humo, vinamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki na vingi viko katika maeneo ya vijijini, huko ambako wengi hawataki kwenda kutokana na ukata wa wananchi. Kanisa limeendelea kutoa huduma makini kwa wagonjwa na waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, limeendelea kuwekeza zaidi na zaidi katika maendeleo ya teknolojia ya habari, sekta inayoratibiwa na Idara ya habari na mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia. Kanisa linamiliki na kuendesha vituo 7 vya Radio, vituo 5 ni vya majimbo na 2 ni vya Mashirika ya kitawa. Baadhi ya majimbo yameanzisha mchakato wa kutaka kufungua vituo vya Radio, ili kuliwezesha Kanisa kuwa ni sauti ya kinabii kwa kuwatetea wanyonge.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.