2014-12-18 09:07:57

Papa Francisko ni mjenzi wa madaraja yanayowaunganisha watu!


Askofu mkuu Thomas Wenski wa Jimbo kuu la Miami, Marekani amewapongeza Marais wa Marekani na Cuba kwa kufanya maamuzi makubwa kwa kurejesha tena uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili; tukio ambalo linaacha kumbu kumbu ya kudumu katika maisha ya watu.

Marais wa Cuba na Marekani wanapongeza jitihada za makusudi zilizofanywa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amejielekeza zaidi katika ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha na kuwaunganisha watu kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni mjumbe na chombo cha amani na majadiliano kati ya watu, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Kanisa Katoliki kwa miaka mingi limekuwa likipinga vikwazo vya uchumi dhidi ya Cuba kwamba, vilikuwa vimepitwa na wakati.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Wenski kwamba, Serikali ya Cuba itaendeleza mchakato wa maboresho ya mahusiano ya kidiplomasia na Marekani, kwa kujikita katika kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu pamoja na demokrasia. Rais Barack Obama wa Marekani amesikika akisema kwamba, kuombea Cuba ianguke si siasa njema, kwani Cuba inahitaji kufanya mabadiliko yatakayowakirimia wananchi wake matumaini, amani na maendeleo ya kudumu.All the contents on this site are copyrighted ©.