Onjeni upendo wa Kristo, ili kuwashirikisha wengine!
Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Watoto wa Umoja wa Vijana Wakatoliki
kutoka Italia waliofika mjini Vatican Alhamisi, tarehe 18 Desemba 2014 amewashukuru
na kuwapongeza pamoja na kuwataka kusonga mbele kwa imani, matumaini na ujasiri mkubwa
katika kugundua mpango wa Yesu katika maisha ya kila mtoto. Dhamana hii wanaitekeleza
kwa kushirikiana na wazazi, marafiki, wenzi wa Katekesi na Michezo.
Baba Mtakatifu
anawataka watoto hawa kuonesha kwamba, wanawajali watoto wenzao ambao wanaogelea katika
umaskini na mazingira magumu ya maisha, kama kielelezo cha mapendo kwa jirani, ili
kweli hija ya maisha yao iweze kujikita katika upendo. Watoto wanapaswa kulipenda
Kanisa na viongozi wake pamoja na kujiweka tayari kuhudumia, kwa kushirikisha muda,
nguvu, vipaji katika maisha na utume wa Parokia, ili kuonesha ushuhuda wa utajiri
ambao Mwenyezi Mungu amewakirimia, ili kuwashirikisha na kuwaonjesha wengine.
Baba
Mtakatifu anawataka watoto kuwa ni mitume wa amani na utulivu kwa kuwamegea jirani
zao upendo, wakiwa wameungana na Yesu, kwa kufanya hivi, kila jambo linawezekana.
Watoto wajenge na kuimarisha utamaduni wa kuzungumza na Yesu kwani yeye ni chemchemi
ya furaha; msamaha na huruma wanapokosa, ili waweze kusimulia matendo makuu ya Mungu
katika maisha yao. Noeli iwasaidie watoto hawa kuwa kweli ni mitume wa Yesu, kwa kumkubali
katika maisha yao, kama alivyofanya Bikira Maria, alipokubali kuwa ni Mama wa Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.