2014-12-18 08:49:06

Miaka 78 ya Papa Francisko, moto wa kuotea mbali!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 17 Desemba 2014 ameadhimisha kumbukumbu ya miaka 78 tangu alipozaliwa. Tukio hili, limewashirikisha watu mbali mbali kwa kukutana kwanza kabisa na baadhi ya maskini kutoka Roma na kuwapatia zawadi kama kumbu kumbu ya tukio hili muhimu katika historia ya maisha yake.

Rais Giorgio Napolitano wa Italia ni kati ya viongozi wakuu wa nchi waliomtumia salam na matashi mema Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuwashirikisha Watu wa Mataifa ujumbe wa amani na matumaini; mambo msingi yanayoacha chapa ya kudumu katika mioyo ya watu. Serikali ya Italia na Kanisa, wataendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu amepokea pia mafuriko ya salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia bila kusahau kwamba, waamini na watu wenye mapenzi mema wametolea sala na maombi yao kwa ajili ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican uligeuka kuwa ni ukumbi wa dansi, watu walipoamua kujimwaga uwanjani na kuanza kucharaza muziki wa "tango" kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko anapomshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai.

Kardinali Claudio Hummes, akizungumza kutoka San Paolo, Brazil, amemtakia Baba Mtakatifu Francisko heri na baraka kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 78 tangu alipozaliwa. Anamsihi asonge mbele kwa ujasiri, imani na matumaini katika mchakato wa kuleta mageuzi makubwa ndani ya Sekretarieti ya Vatican kama walivyoshauri Makardinali katika mikutano yao elekezi, bila ya kukata tamaa, kwani Familia ya Mungu iko nyuma yake.

Kardinali Claudio Hummes amemtakia afya njema, furaha na amani anapotekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, hata kama kuna ugumu na changamoto zake. Kardinali Hummes anatambua uzito na unyeti wa utume huu, lakini asiogope, waamini wanaendelea kumkumbuka na kumsindikiza kwa sala na sadaka zao, ili yote yafanyike kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu pamoja na ustawi wa Kanisa la Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.