Kardinali Antonio Maria Veglio’, Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji
kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum anasema kwamba, katika kipindi
cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko la kundi kubwa la watoto wanaotumbukizwa
katika biashara haramu ya binadamu na uhalifu wa kimataifa.
Hawa ni watoto
ambao wamepokwa utu, heshima na matumaini yao kwa siku za usoni, kwani hakuna mtu
anayewajali na kuwatunza na matokeo yake ni kwamba, wanaishia pabaya kama askari ambao
ni chambo kinachopelekwa mstari wa mbele katika mapambano; ni watoto kama hawa wanaohusishwa
katika biashara haramu ya dawa za kulevya na ukahaba.
Watoto hawa anasema
Kardinali Veglio’ hawana ulinzi wala tunza kutoka kwa wazazi au walezi wao, ni watoto
ambao wamekimbia vita,umaskini, nyanyaso na adha mbali mbali za maisha. Kanisa kwa
kutumia taasisi zake mbali mbali limekuwa mstari wa mbele kuwasaidia na kuwahudumia
watoto wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, mada
ambayo kwa sasa inavaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwani huu ni uhalifu dhidi
ya ubinadamu.
Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na watu wote
wenye mapenzi mema ili kutoa taarifa kamili juu ya biashara haramu ya binadamu na
utumwa mamboleo, mwenendo na tabia yake pamoja ya kupinga ukosefu wa haki msingi dhidi
ya watu kama hawa.
Serikali zikiwa na sera makini juu ya wahamiaji, zinaweza
kushirikiana kikamilifu na Kanisa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia
na kuheshimu utu wao kama binadamu na wala si kama mzigo na chanzo cha kampeni chafu
dhidi ya wahamiaji, kama inavyojionesha katika nchi nyingi za Ulaya. Hivi karibuni,
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani wameunganisha nguvu zao na Baraza la Maaskofu
Katoliki Mexico, ili kutekeleza mikakati ya pamoja kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji
kutoka Mexico; ili kulinda na kutetea utu na heshima ya wakimbizi na wahamiaji hawa,
ambao wakati mwingine wanakumbana na “Pazia la chuma”.
Kuna idadi kubwa ya
watoto wanaoteseka kutokana na kukosa wazazi na walezi wakati wanapokuwa uhamishoni,
matokeo yake wanajikuta wakiishia kwenye magereza ya watoto, hali ambayo inawachia
madonda makubwa katika maisha na makuzi yao, hili kwa upande mwingine anasema Kardinali
Antonio Maria Veglio’ kuwa ni janga la kimataifa, hali ambayo kamwe haiwezi kukubalika
iendelee kama ilivyo.
Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, watoto hawa wanapokelewa
na kupewa hifadhi kisheria sanjari na kuendeleza marekebisho katika sheria juu ya
wahamiaji pamoja na kusaidia kupambana na mambo yanayopelekea kundi kubwa la watoto
kukimbia kutoka kwa wazazi wao. Kwa maneno mengine, kuna haja ya kusaidia mchakato
wa kupambana na umaskini ambao ndicho chanzo kikuu kinachowafanya watu wengi kukimbia
nchi zao.
Watoto wengi wanaishi katika mazingira hatarishi, kiasi kwamba,
wanakumbwa na kishawishi kikubwa cha kukimbia ili kutafuta maisha bora zaidi hata
kwa gharama ya maisha yao na matokeo yake, wengi wao wanakufa maji baharini au kwa
kiu na utupu jangwani.
Baadhi ya watoto hawa anasema Kardinali Veglio’ wanatumbukia
kwenye mikono ya wafanyabiashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, hivyo wanauzwa
kama biadhaa Barani Ulaya mambo yanayodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu.
Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimsiha kumbu kumbu ya miaka 25 tangu Azimio la Haki ya
Mtoto lilipoanzishwa kunako mwaka 1989, kuna haja ya kuendelea kukazia umuhimu wa
watoto kutobaguliwa wala kutengwa, kwa kuhakikisha kwamba, haki za watoto zinalindwa
na kudumishwa kwa kupatiwa: elimu, afya pamoja na kuungana na wazazi wao.
Takwimu
zinaonesha kwamba, watoto wadogo ambao ni wakimbizi na wahamiaji, wengi wao ni kutoka
Kusini mwa Jangwa la Sahara, yaani Eritrea, Somalia na Sudan na wengine wanatoka Mashariki
ya Kati, huko ambako vita, nyanyaso na kinzani za kidini na kisiasa bado zinapamba
moto. Watoto hao wanafanya maamuzi magumu yaliyo juu ya uwezo wao, kumbe, wanapaswa
kusikilizwa kwa makini, kupewa tiba na kusaidiwa kuwa na matumaini ya leo na kesho
iliyo bora zaidi kuliko walikotoka. Maisha ya watoto hayana budi kupewa kipaumbele
cha kwanza badala ya mtindo wa sasa wa kuangalia idadi yao, kwani nyuma ya idadi,
kuna utu na haki msingi za watoto.
Kardinali Antonio Maria Veglio’ anawashukuru
wadau mbali mbali wanaojitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia watoto wahamiaji
na wakimbizi kupata tena matumaini mapya, kwani watoto wanapokubalika na kupolekewa;
wanapopendwa na kuheshimiwa; wanapohudumiwa na kulindwa, hapo jamii inaboreka zaidi
na kuwa na uhakika wa amani, usalama na utulivu, vinginevyo, itakuwa ni patashika
nguo kuchanika!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican.