Jifungeni kibwebwe kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa!
Tanzania inapoendelea kusherehekea Miaka 53 tangu ilipojipatia uhuru wake wa bendera
kutoka kwa Mwingereza inayo mambo mengi ya kujivunia, hata kama bado kuna changamoto
nyingi zinazowakabili watanzania. Bwana Salvatory Mbilinyi, Afisa kutoka Ubalozi wa
Tanzania nchini Italia katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Tanzania
imepiga hatua kubwa katika mchakato wa kuwaletea watu wake maendeleo endelevu!
Kuna mafanikio
makubwa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya watu yaliyokwisha kupatikana nchini
Tanzania kupitia katika Serikali za awamu mbali mbali. Kuna haja ya kuendelea kudumisha
misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa kwa kutambua kwamba, wote ni watanzania
na tofauti zao za kidini kisiwe ni kisingizio cha chuki na uhasama. Watanzania wanapaswa
kuendelea kujibidisha zaidi katika maboresho ya kiuchumi kwani hii ni changamoto kubwa
kwa watanzania wengi kwa nyakati hizi.