2014-12-17 08:45:14

Watawa na ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana kwa makini!


Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Jumanne, tarehe 16 Desemba 2014 limezindua taarifa ya kazi ya kitume iliyofanywa kwenye Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yenye hadhi ya Kipapa na Kijimbo nchini Marekani kwa kuwahusisha watawa wengi kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2012.

Taarifa hii imewasilishwa kwa waandishi wa habari mjini Vatican na Kardinali Joao Braz de Avis, Rais wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na viongozi waandamizi kutoka katika Baraza na Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume. Mkutano huu umehudhuriwa pia na viongozi wa watawa kutoka Marekani. Watawa wamepewa kwa mara nyingine tena fursa ya kugundua ndani mwao mpango wa kazi ya ukombozi na matunda ya mawasiliano kati ya watawa, viongozi wa Kanisa na waamini walei.

Majadiliano ya kina yanayoendelea kati ya watawa yanapania kuimarisha na kudumisha uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa mintarafu karama za waanzilishi wa Mashirika yao. Kardinali De Avis anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya Mashirika ya kitawa yalikataa kuonesha ushirikiano, ingawa bado kuna nafasi ya kuendeleza majadiliano katika ukweli, uwazi na heshima kwa mashirika kama haya!

Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linaendelea kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuhakikisha kwamba, watawa wanashirikishwa kikamilifu katika mchakato wa kujadili, kuamua na kutekeleza masuala yanayohusu maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni fursa nyingine ya kujipatanisha, ili watawa waweze kuwa kweli ni mashuhuda angavu, wanaoonesha mvuto na mashiko katika umoja na udugu.

Kwa upande wake Askofu mkuu Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume amefafanua kwamba, Mashirika yaliyohusika zaidi ni yale yanayotekeleza wito na utume wake nchini Marekani kwa kuwa na Makao yake makuu; Makao makuu ya kanda au nyumba ya malezi na kwamba, jumla ya Mashirika 405 yametembelewa na kukaguliwa na Sr. Mary Clare Millea, kiongozi wa kitume aliyekuwa ameteuliwa na Baraza la Kipapa kutekeleza dhamana hii kwa kushirikiana na jopo la watawa.

Jopo hili limefanya upembuzi yakinifu kuhusiana na uelewa kuhusu maisha ya kitawa na kazi za kitume nchini Marekani mintarafu majadiliano ya kina. Utamaduni wa kusikiliza watawa kwa makini ni kati ya mambo yaliyopewa kipaumbele cha pekee katika utekelezaji wa dhamana hii, ili kutambua utajiri wa urithi wao, changamoto zilizopo, matumaini yao kwa siku za usoni na mazingira ya maisha na utume wa Kanisa mahalia!

Ukaguzi huu umefanyika katika hatua kuu nne: kwa kufanya majadiliano ya kina na wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume na baadaye wakuu wa Mashirika walipewa dhamana ya kujaza taarifa kuhusiana na ubora wa maisha ya kitawa, kijumuiya na kitume kwa kila mtawa. Sr. Millea amewasilisha taarifa ya jumla kuhusiana na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Marekani: kuhusiana na mwelekeo wa Mashirika haya.

Hii imekuwa ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano, umoja na udugu kati ya watawa, viongozi wa Kanisa na waamini walei na wengi wa wakuu wa Mashirika ya kitawa wamekubaliana kimsingi na upembuzi yakinifu uliofanywa na Jopo hili. Watawa wamechunguza dhamiri zao mbele ya Neno la Mungu; majadiliano ya maisha ya kiroho mintarafu maisha, ushuhuda na utajiri kutoka kwa waanzilishi wa Mashirika haya bila kusahau mchango wao katika nyaraka mbali mbali za Kanisa.

Watawa wanakiri kwamba, kumekuwepo na mshikamano wa dhati kati ya watawa wa kike na upendo wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; mambo yanayooneshwa pia na wakleri pamoja na waamini. Watawa wanaendelea kuhamasishwa kuchangia kwa hali na mali utajiri mkubwa walionao watawa katika Mashirika yao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na huduma kwa Kanisa. Watawa wanasema, wataendelea kushikamana kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kwa kukuza uhuru wa kidini na kidhamiri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.