2014-12-17 15:51:34

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili IV ya Kipindi cha Majilio


Ni mara nyingine tena tunakutana kushirikishana furaha na mapendo ya Mungu kwa njia ya Neno lake. Ni Dominika ya nne ya Majilio, tunapoelekea sherehe za Noeli, sherehe za kuzaliwa Mtoto Yesu, Mtoto Emanueli yaani Mungu pamoja nasi. Katika masomo ya Misa, Dominika ya nne tunapata ujumbe ukituambia kuwa, Yesu ndiye Masiya wa kweli tuliyehaidiwa tangu zama za mababu zetu. RealAudioMP3

Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha pili cha Samweli tunapata ujumbe wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika ukoo wa Daudi na kwa jinsi hiyo ukoo wa Daudi utatawala milele. Mfalme Daudi anawaza kumjengea nyumba mwenyezi Mungu lakini badala yake Mungu anamwambia Nabii Nathani akamwambie Daudi kuwa yeye hawezi kumjengea nyumba Mungu, bali Mungu mwenyewe atamjengea nyumba Daudi.

Ndiyo kusema katika ukoo wa Daudi atazaliwa Mwana wa Mungu. Na hivi ukoo huu utakuwa na jina kuu kupita majina mengine na mwisho nyumba ya Daudi na ufalme wake vitathibitishwa milele. Habari hii haiwezi kuwa habari ya kawaida bali kuzaliwa kwa Masiya, Mkombozi wa ulimwengu.

Ni katika mantiki hiyo ya kukuzwa kwa ufalme wa Daudi yaani kuzaliwa Masiya, Mtume Paulo anatoa shukrani kwa Mungu kwa zawadi hiyo kubwa ya kumpata mkombozi. Anawakumbusha Warumi wamtukuze yeye tu, ambaye huwafanya imara, aliye hekima kamilifu peke yake. Kwa jinsi hiyo, atuonya nasi daima kumtukuza Mungu na kumpa sifa, yeye peke yake na aliye mweza wa yote.

Mwinjili Luka anakaza ujumbe tunaoupata katika somo la kwanza. Tunamwona malaika Gabrieli akipeleka ujumbe wa Mungu kwa mwanamwali Bikira Maria kwamba atamzaa Mwana wa Mungu. Mwanamwali huyu alikuwa ameposwa na Yusufu wa ukoo wa Daudi. Anashangaa habari ya malaika Gabrieli, lakini kwa neema ya Mungu anaitika: Nitendewe kama ulivyonena. Mungu anamjengea nyumba mfalme Daudi na ufalme wake na nyumba yake vinathibitishwa milele.

Kumbe sasa ufalme wa Daudi uliokuwa wa muda unachukuliwa na mfalme mwenyewe wa milele aliyekuwa amempa mfalme Daudi kutawala kwa muda, Mfalme huyu ni Kristu Masiya. Mpendwa, ni kwa mantiki ya ufalme mpya nasi tunaalikwa kujiweka katika ufalme huo na si tu kujiingiza huko tu, bali kujiachia kuongozwa na ufalme huo yaani Yesu Kristo Mkombozi, dira na kiongozi wa ulimwengu mpya.

Mpendwa, habari hii ya furaha ni kwa ajili yako, malaika anapiga hodi kwako kila mara akisema utampokea Bwana katika Ekaristi takatifu! Yakupasa kuitikia ukisema nitendewe kama unavyotaka! Habari ya furaha ya kuzaliwa Masiya umeipata tangu Dominika ya I ya Majilio na ukaendelea nayo mpaka sasa! Unasemaje? Mimi nasema Bwana nitendewe kama ulivyonena, njoo Masiya ukae nasi, njoo ukatuokoe, ushukie Masiya kuwaokoa watumwao! Emanueli kaa nasi Bwana.

Ninakualikeni kumpenda Mama Bikira Maria ambaye alikuwa Tabernakulo ya kwanza akimbeba mtukuka Mwana wa Mungu, mkombozi wa ulimwengu. Ni kwa njia ya Bikira Maria mtoto Emanueli, mkate wa Mbinguni umetufikia.

Tumsifu Yesu Kristo na Maria.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.