2014-12-17 15:04:28

"Suprise kwa Manongayembe"! Ya Leo Kali!


Msichana asiyeolewa hana hadhi ya kuitwa mke, na ni mbaya zaidi kama hana mtoto, dada huyo hawezi kamwe kuitwa mama. Kuna wimbo wa ngoma ya madogoli ya vijana wa kingoni unamwimba msichana aliyekuwa anakataliwa na kila mvulana: “Vijana wa Maposeni wamekukataa! Vijana wa Nambarapi, Wamekukataa! Vijana wa Mfaranyaki, Wamekukataa! Vijana wa Bombambili! wamekukataa! Njoo huku nikuoe mimi!”


Aibu ya mtindo huo ilimkumba pia binti mmoja tutakayemsikia katika Injili ya leo. Ingawaje binti huyo alikuwa ameposwa na bwana, lakini bado alijisikia kunyanyasika kwa sababu hakuwa na mtoto. Mungu bariki, akapata mtoto wa kiume. Unyonge ukamwishia na akajisikia kuwa mtu mbele ya watu.
Kabla ya kusikia kimbembe kilichompata binti huyo budi ieleweke kuwa, habari tutakayoisikia siyo michapo na siyo masimulizi ya kihistoria. Kwa sababu kama ni michapo, basi tusipotezeane muda kusikiliza.


Kama ni historia ya kweli basi mtaona pia jinsi ilivyosimuliwa kuwa inaleta utata na udadisi. Mathalani, unaweza kuuliza, “huyo binti alikaa wapi na alikuwa anafanya nini? Halafu utasikia pia wakati anataarifiwa kwamba atapata mtoto, akachanganyikiwa na kuogopa kupata mimba. Kwa sababu gani aliogopa endapo alishaolewa na alitegemea kuwa na familia? Halafu yule mjumbe aliyempasha habari zile aliingiaje mle chumbani alimokuwa mke wa mtu? Kadhalika, kwa nini binti mwenyewe asimtonye mumewe kwamba yu mjamzito au katokewa na amepata ujumbe wa faragha?


Ndugu zangu, ukitaka kuifaidi habari ya binti huyu, budi umwelewe mwandishi alikuwa ni mtu wa namna gani na anataka kutuambia nini. Mwandishi huyu alikuwa gwiji wa Maandiko Matakatifu na mtaalamu aliyebobea katika mambo ya Manabii wa Agano la Kale na aliyeweza kuwanukuu kirahisi na kuyaweka maneno ya manabii hao kwenye kinywa cha malaika. Hebu tumfuatilie mtaalamu huyu anavyomwelezea binti huyu bikira na mambo yaliyompata.


Mwandishi anapotaka kusimulia mwanzo wa kituko cha kihistoria, anatuambia kuwa kilianza “Mwezi wa sita.” Mwanzo huu muhimu sana, umefasiriwa itakiwavyo katika biblia ya Kiswahili lakini bahati mbaya katika Misale ya Kiswahili maneno hayo muhimu yameachwa.


“Mwezi wa sita” unatueleza maana ya kitaalimungu kuliko ya historia au mchapo. Angalia tu kuwa hata binadamu wa kwanza aliumbwa siku ya sita. Ulikuwa pia mwezi wa sita tangu Elizabeti alipotunga mimba ya Yohane Mbatizaji. Sasa unatajwa tena kuonesha mwanzo wa historia mpya ya ukombozi.


Mwinjili anaendelea kutuambia kwamba mwezi huo wa sita, “Malaika alitumwa kwenda Galilea katika mji wa Nazareti.” Katika Agano la Kale kijiji hicho hakitajwi kabisa kutokana na udogo wake. Hata Natanaeli anakidharau sana aliposema: “Laweza neno jema kutoka Nazareti.” Katika kijiji hicho waliishi watu wa kawaida kabisa. Kumbe uchaguzi wa Mungu ni kwa vitu vidogo.


Kisha Mwinjili anatupeleka kwenye wazo lake kuu anaposema: “Kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na Yosefu, jina lake bikira huyo ni Maria.”Neno hilo Bikira linatajwa hapa mara mbili ili kuonesha msisitizo. Hebu tuuangalie ubikira huo unamaanisha nini na unamhusu nani? Katika agano la Kale ubikira haukuwa na thamani kwa mwanamke kama tunavyoufikiria sisi leo. Watu wa kale hata kwa waafrika, jambo lenye thamani sana kwa mwanamke ni kuzaa, yaani kuwa na watoto tena watoto wengi ndicho kitu pekee kinachompa mwanamke heshima ya kuitwa mama. “Mke wako atakuwa kama mzabibu wenye kuzaa ndani ya nyumba yako ( ).

Jina Bikira liko katika hali ya kike na lilitumika hasa kuwaita waisraeli au taifa la kiyahudi au Waisraeli hasa pale walipokuwa utumwani, wanyonge wasiojulikana na wakinyanyaswa na mataifa makubwa. Kwa hiyo bikira ni jina linalosimama kuonesha hali ya mwisraeli aliyepigika na kunyenyekeshwa: “Bikira binti Sayuni, anakudharau, anakudhihaki sana; binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake juu yako.” (Isaya 37:22).

Nabii Yeremia analia: “’Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana, wala yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu, kwa jeraha isiyoponyeka.” (Yeremia 14:17). “Usizidi kufurahi ewe bikira uliyeaibishwa, binti wa Sidoni. Haya ondoka, uende hata Kitimu; huko nako hutapata raha” (Yer. 23: 12).


Kwa hiyo mwinjili anaposisitiza juu ya ubikira wa Maria, hamaanishi tu ubikira wa kimwili, kama aliokuwa nao kabla ya kukaribiana na Yosefu, bali anataka kuzungumzia ubikira mwingine. Kama vile ulivyokuwa utasa wa Elizabeth ulivyomaanisha ukavu, uchungu na umaskini wa maisha ya kibinadamu, kadhalika ubikira wa Maria kuwa “manonga yembe”, yaani kukosa Bwana, kudharaulika, kunyongeka, kunyanyasika na kunyenyekeshwa kwa msichana. Maria anapotunga mimba anafurahi na anaimba utenzi: “Moyo wangu wamtukuza Bwana na roho yangu imeshangilia katika Mungu Mkombozi wangu” kwa hoja kwamba Mungu “Ameangalia unyenyekevu wa mtumishi wake (Israeli), Amenitendea makubwa aliye mwenyezi. Yaani, we “mwache Mungu aitwe Mungu.” Amewaacha wakuu, wenye uzuri, warembo akaja kuvutika na mimi mnyonge wa kutupwa.


Sasa unaona huyo binti Sayuni ameachana na utumwa, na manyanyaso ambayo ni ubikira wake, sasa anakuwa mama. Kisha mwinjili analitaja jina la bikira: “na jina la Bikira huyo ni Maria.” Jina hili Maria siyo geni. Lilijulikana na kupendwa Galilea nzima. Maria alikuwa ni mmojawapo wa wasichana wengi waliokuwa wanaitwa hivyo ,kwani wakati huo jina hili lilipendwa sana, na karibu katika kila familia kulikuwa na binti walau mmoja aliyepewa jina la Maria. Kwa mfano tunasikia kuna Maria Magdalena, Maria wa Kleopa, Maria wa Yakobo, Maria wa Betania, Maria aliyependwa sana na Herode. Maria dada ya Lazaro na Marta nk. Jina hili kwa kiyahudi ni rum ram lenye kumaanisha “aliyetukuka, binti mfalme”. Ama kweli ni jina zuri linalomfaa mzazi wa Mungu. Baada ya kulitaja jina hilo sasa malaika anamsapraizi Maria na kumwambia: “Ufurahi Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe.”


Neno hili “Ufurahi” katika Agano lakale linamhusu Israeli. Ndiye yeye anayealikwa kufurahi. “Imba, ee binti Sayuni, piga kelele, ee Israeli; furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yeruslemu; (Sefania 3:14) Kadhalika “Imba, ufurahi, ee binti Sayuni, maana, tazama, ninakuja, nami nitakaa kati yako, asema Bwana” (Zekaria 2:10). Huyu “Binti Sayuni” kilikuwa kinaitwa kijiji fulani kidogo sana kilichokuwa kaskazini mwa Yerusalemu. Katika kijiji hicho waliswekwa mateka waisraeli (wayahudi) waliotoroka utumwani. (Israeli Hezekia). Katika kijiji hicho kuikithiri ufukara kupita vijiji na miji mingine yote. Kijiji hicho kiliitwa “Binti Sayuni” na kililinganishwa na tumbo la uzazi, kwamba katika tumbo la bikira, binti Sayuni atazaliwa mtoto. Sasa binti huyo anayefurahi.


Kwa hiyo “sapraizi” hiyo si ya Maria pekee yake, bali ni ya Waisraeli wote, na sanasana ni ya watu wote ulimwenguni, wanaonyanyaswa, wanashushuriwa, wanaonyenyekeshwa, wanaokosewa haki, wanaokosa upendo na wanaokosewa utu wao. Watu hao ndiyo akina binti Sayuni. Sasa wanaambiwa furahini, kwani mmependwa na Bwana. Kwa maneno hayo, Maria anaogopa na anauliza: “Kulikoni amkio hili.” Kisha anaambiwa “usiogope.” Hili ndilo linalotumika daima na Mungu kwa mtu anayetaka kumtuma kazi: “Usiogope mimi niko nawe. Tazama utatunga mimba na kupata mtoto utakayemwita Yesu.” Anaongeza kusema kwamba, “Mtoto huyo atakuwa mkuu, Mwana ,wa aliye juu kabisa.”


Kisha Maria anauliza “Je itakuwaje? Tafsiri ya swali hili ni tofauti na alichokitunga Mtakatifu Augustino, kwamba Maria aliuliza hivyo kwa lengo la kutaka kutunza ubikira wake, la hasha, kwa vile kama bikira Maria angetaka kubaki bikira angeenda kuingia utawa wa Waeseni waliokuwa hapo jirani. Kinyume chake ni kwamba Marua mwenyewe aliamua kuolewa na Yosefu ili apate watoto. Kwa hiyo kwa swali hilo, Maria anataka kujua, utume wake ni upi? Kisha malaika anasema: Shughuli hiyo ni ya Roho mtakatifu, yaani, kazi ya uumbaji kama ilivyo katika kitabu cha mwanzo ni kazi ya Roho mtakatifu.


Kisha Maria anatoa jibu linalokomeshea: “Ndimi mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena.” Neno hili “Ndimi” linayosikika mara 178 katika biblia yote kutoka kwa wale wanaoitwa na Mungu. Kwa mfano Ibrahimu, Isaya, Samweli nk. Yesu alikuwa wa kwanza kuitikia “Ndimi” kisha akatumwa na Mungu Baba yake kuja duniani, siyo kwa ajili ya kutumikiwa bali kutumikia. Akawa binadamu mnyonge lakini mwishoni akakuzwa sana. Nawe katika maisha yako ya kinyonge daima ujibu“Niko Bwana nitume mimi” kisha utatukuzwa pamoja na Kristo.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.