2014-12-17 14:39:07

Familia Takatifu! Happy Birth Day!


Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Wito na Utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo" ameamua kuandaa Katekesi kuhusu Familia na siku ya Jumatano tarehe 17 Desemba 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameanza na Katekesi kuhusu Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Kipindi cha Majilio anasema Baba Mtakatifu ni wakati wa sala kwa ajili ya kumngojea Mwana wa Mungu anayezaliwa duniani, mwaliko kwa waamini kuangalia kwa umakini mkubwa jinsi ambavyo zawadi ya Mungu kuhusu familia ilivyopewa thamani ya hali ya juu kiasi cha kufumbwa katika Fumbo la Umwilisho. Mwana wa Mungu akaamua kuzaliwa katika Familia ya binadamu, katika mji usiofahamika, pembezoni kabisa mwa Utawala wa Ufalme wa Kirumi.

Baba Mtakatifu anasema, Injili inasimulia kidogo sana kuhusu maisha ya Yesu katika kipindi cha miaka thelathini ya maisha yake hapa duniani, lakini inasadikika kwamba, Yesu aliishi kama kawaida ya watu wa nyakati zake. Alizaliwa na kulelewa katika mazingira ya familia ya watu waliokuwa na ibada, akajifunza kutoka kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya maisha Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, hapo akakua katika kimo, hekima na neema.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa Familia Takatifu katika maisha na utume wao kwa kumwandalia Yesu makao katika nyumba zao. Ni kwa njia ya ushuhuda wa upendo unaobubujika kutoka kwenye familia za kawaida, upendo wa Mungu unaweza kuwafikia na kukaa na wengi, ili kuukomboa ulimwengu.

Baba Mtakatifu anawatakia kheri na baraka kwa Siku kuu ya Noeli, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, changamoto na mwaliko kwa waamini kutafakari kwa kina kuhusu Familia kuwa ni mahali ambapo Yesu alipata zawadi ya maisha akaikuza na kuidumisha. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaomwombea wakati huu anapofanya kumbu kumbu ya miaka 78 tangu alipozaliwa pamoja na kumtakia kheri kwa Siku kuu ya Noeli.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kutoka Mashariki ya Kati kwamba, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu alijinyenyekesha, akawa mdogo na fukara, ili aweze kuwa sawa na binadamu katika mambo yote isipokuwa dhambi. Bikira Maria awasaidie waamini kutambua sura na mfano wa Mungu kutoka kwa jirani zao, lakini zaidi kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Noeli na Mwaka Mpya zitakuwa ni siku za furaha, wema na amani, kwa kutoa nafasi kwa Mfalme wa Amani ili aweze kung'ara tena katika maisha ya watu, kwa kuzikirimia familia matumaini na mapendo. Kipindi cha majilio na hatimaye Noeli, iwe ni fursa ya kusali zaidi na kumwilisha sala hii katika matendo ya huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.