2014-12-16 07:54:23

Wakatoliki nchini Uingereza wameamua kujitosa kimasomaso katika mchakato wa Uinjilishaji mpya!


Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuunga mkono changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji, kwa kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha.

Wakristo wote wanapaswa kushiriki kikamilifu katika azma ya Uinjilishaji kwani hii ni sehemu ya wajibu wao msingi. Lengo ni kuwawezesha Wakristo kutekeleza wajibu wao wa Kimissionari kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na yenye mvuto. Parokia ishirini na mbili zimetengwa maalum ili kuhamasisha waamini kushiriki katika mradi huu mkubwa wa Uinjilishaji kwa ajili ya Mwaka 2015.

Watu wana kiu ya kusikiliza Neno la Mungu sanjari na kuonjeshwa imani inayojikita katika matendo. Maaskofu wanataka kutekeleza kwa matendo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Injili ya Furaha, kwa kujikita katika dhamana ya Uinjilishaji, ili kuwashirikisha watu furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Tarehe 11 Julai 2015 kutafanyika mkesha wa sala na kongamano la kitaifa kuhusu Uinjilishaji mpya! Waraka wa Injili ya Furaha ni dira na mwelekeo mpya unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, kwa kujitahidi kukutana na Yesu katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Parokia mbali mbali zinapania kuwashirikisha waamini walei ili kuunda kikosi kazi kitakachohamasisha mchakato wa Uinjilishaji mpya, mwaliko na changamoto kwa waamini kushiriki kikamilifu katika mradi huu mkubwa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.All the contents on this site are copyrighted ©.