2014-12-16 08:52:54

Ukabila chanzo cha vita na kinzani Sudan ya Kusini!


Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, tarehe 15 Desemba 2014 imeadhimisha kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu machufuko yalipotokea nchini humo na hivyo kusababisha maafa na mahangaiko makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia, kutokana na misigano ya kisiasa na uchu wa mali na madaraka. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 50, 000 waliathirika vibaya kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini.

Askofu mkuu Paolino Lukudu Loro, wa Jimbo kuu la Juba, amewataka wananchi na watu wote wenye mapenzi mema Sudan ya Kusini, kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani na utulivu, huku wakiomba msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtafaruku kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa Makamu wa Rais Riek Machar, ulifumuka kunako tarehe 15 Desemba 2013 huko Juba na tangu wakati huo, machafuko haya yakapata shinikizo la ukabila na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini imesababisha zaidi ya watu millioni mbili kukosa makazi, hali ambayo ilipelekea kuchechemea kwa uchumi wa Sudan ya Kusini. Hadi sasa zaidi ya watu 572 wametambulika kuwa walipoteza maisha wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto wadogo linalaani kitendo cha makundi yanayosigana huko Sudan ya kusini kupeleka watoto wenye umri chini ya miaka kumi na miwili, mstari wa mbele katika mapigano; mambo ambayo yanahatarisha ustawi na makuzi ya watoto hawa kwa siku za usoni. Licha ya mchakato wa kutaka kupata suluhu na amani ya kudumu nchini Sudan ya Kusini, lakini wachunguzi wa mambo wanasema, bado mambo hayakamilika sawa sawa!







All the contents on this site are copyrighted ©.