2014-12-16 10:29:43

Majadiliano katika ndoa ni muhimu sana, ili kudumisha amani na utulivu!


Msingi wa familia uko katika uamuzi na chaguo la hiari la wawili kuunganika katika Sakramenti ya Ndoa, kwa kuzingatia maana na thamani ya taasisi, yaani familia, jambo hili halimtegemei mwanadamu bali Mwenyezi Mungu mwenyewe. Hakuna mwenye uwezo wowote wa kumwondolea mtu haki asili ya Ndoa au kufanya mabadiliko katika tabia, sifa na lengo lake.

Kwa kawaida Ndoa imejaliwa kuwa na sifa ya kudumu inayojikita katika: ukamili ambamo wawili, mume na mke, wanajitoa mmoja kwa ajili ya mwingine katika hali zote za kiutu, kimwili na kiroho; umoja ambao huwafanya wawe mwili mmoja; udumifu na uaminifu. Huu ndio mpango wa maisha ya ndoa katika maisha ya mwanadamu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, Wabatizwa wanaishi hali halisi ya urithi wa mwanadamu wa ndoa katika Umungu wa Sakramenti, Ishara na chombo cha neema.

Sakramenti ya ndoa inabeba uhalisia wa mwanadamu wa upendo wa kindoa katika maana kamili na uwajibikaji zaidi, kwani wanatambua kwamba, wao ni Kanisa dogo la nyumbani. Mwanadamu ameumbwa katika upendo na kamwe hawezi kuishi pasi na upendo. Familia ni mahali pa kutakatifuza maisha; kuelimisha na kudumisha: imani, mapendo na matumaini. Familia ni mahali pa kujifunza kutoa na kupokea msamaha wa dhati unaobubujika kutoka katika undani wa maisha ya wanandoa.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, anakazia umuhimu wa wanandoa kujifunza utamaduni wa kusikilizana. Majadiliano kati ya wanandoa ni jambo muhimu sana, ili kujenga na kudumisha amani na utulivu.All the contents on this site are copyrighted ©.