2014-12-16 12:10:23

Jivikeni: unyenyekevu, ufukara na imani, ili kupata uzima wa milele!


Unyenyekevu ni fadhila inayoweza kumwokoa mwanadamu mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu, lakini kiburi, majivuno na hali ya kujiamini kupita kiasi ni mambo ambayo ni chukizo mbele ya Mwenyezi Mungu. Waamini wanapaswa kujivika vazi la unyenyekevu, kwa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kusikiliza sauti ya Mungu inayozungumza nao kutokana katika dhamiri zao nyofu. Mwanadamu akimgeuzia Mungu kisogo hapo atapata hukumu, lakini akimfungulia moyo wake kwa toba, ataweza kupata maisha ya uzima wa milele!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake siku ya Jumanne, tarehe 16 Desemba 2014 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, kwa kufanya rejea kwenye Liturujia ya Neno la Mungu. Nabii Sefania katika somo la kwanza anaonesha mji wenye udhalimu na maasi, lakini pia Taifa la Mungu linalojikita katika: unyenyekevu, ufukara na imani kwa Mwenyezi Mungu. Wale ambao hawakusikiliza maonyo yaliyotolewa dhidi ya matendo yao maovu watahukumiwa!

Baba Mtakatifu anasema, Injili imehubiriwa kwa Watu wa Mataifa, wale walioisikia na kuimwilisha katika maisha yao, wamekirimiwa uwezo wa kuwa ni warithi wa Ufalme wa Mungu, lakini wale ambao wamejichimbia katika ubinafsi wao, wanaodhani kwamba ni watakatifu kwa vile wanakwenda Kanisani na kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, lakini hawajitaabishi kutubu na kumwongokea Mungu, watashangaa watakapokuta wametupwa nje ya Ufalme wa Mungu, huku wakiwaona watoza ushuru na makahaba, waliotubu wakifurahia uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu; wawe tayari kufundwa na kurekebishwa ili waache mienendo yao mibaya, tayari kumrudia Mwenyezi Mungu, bila ya unafiki wowote ule! Waamini wawe na ujasiri wa kumfungulia Mwenyezi Mungu sakafu ya mioyo yao, kwa kutubu na kumwongokea kutoka katika undani wa maisha yao bila kificho kwani anajua yote yaliyoko sirini.

Matendo mema mbele ya Mungu, yaoneshe pia ujasiri wa kutubu kwa unyenyekevu mbele ya Mungu kwa kutambua kwamba, kama binadamu, daima anaogelea katika dhambi na utupu, kumbe, anahitaji kuonjeshwa huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.All the contents on this site are copyrighted ©.