2014-12-15 08:55:22

Yesu Kristo ni chemchemi ya furaha ya kweli kwa mwanadamu!


Kipindi cha Majilio ni wakati muafaka wa kujiandaa kikamilifu katika maisha ya kiroho kwa ajili ya ujio wa Yesu Kristo na kwa namna ya pekee, kukiishi kipindi hiki kwa kuwa ni watu wenye furaha inayobubujika kutoka kwa Yesu, kwani kwa Yesu, furaha imefika nyumbani na wala hakuna mchezo!

Binadamu anahitaji kuonjeshwa furaha na kwamba, Mkristo anaalikwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anaishuhudia furaha kwa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu ambaye yuko daima katika maisha ya waja wake. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, mwanadamu amepata mbegu ya uwepo wa Ufalme wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kuwaonesha wengine ile furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na utimilifu wa furaha hii ni katika maisha yenye uzima wa milele!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 14 Desemba 2014. Baba Mtakatifu anasema, Yesu Kristo ni chemchemi ya furaha ya watu wake na kwamba, bila Yesu, hakuna furaha ya kweli, kwani Yesu aliyeteseka, akafa na kufufuka anaendelea kutenda kazi katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.

Wakristo wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanapokea na kukumbatia ndani mwao, uwepo endelevu wa Mungu kati yao sanjari na kuwasaidia wengine kuonja uwepo huo wa Mungu kati yao kama alivyofanya Yohane Mbatizaji. Waamini wawaongoze watu kumwendea Yesu kwani yeye ndiye lengo kuu la maisha kwa binadamu anayetafuta furaha ya kweli.

Baba Mtakatifu anasema, waamini wanaweza kuwa kweli ni Wamissionari wa Furaha kwa kusali bila kuchoka; kwa kumwomba Roho Mtakatifu; kwa kutafuta mema na kuachana na mabaya. Ikiwa kama huu ndio mtindo na mfumo wa maisha, basi hapana shaka kwamba, Habari Njema ya Wokovu inaweza kuingia katika Familia na kuwasaidia watu wengi zaidi, ili kupata amani na utulivu wa ndani hapa pale wanapoelemewa na magumu katika maisha.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuonesha uso wa furaha na tabasamu, kwani ndani mwao kuna chemchemi ya amani na utulivu, hata wakati wa shida na magumu katika maisha na kwamba, imani si kizuizi cha shida! Lakini jambo la msingi ni kutambua kwamba, katika mahangaiko yote haya, bado Mwenyezi Mungu yupo pamoja na wajawake. Mungu ndiye anayewakirimia watoto wake amani.

Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanamshuhudia Kristo, Neno wa Mungu, anayeyaangazia mapito ya mwanadamu; kwa kuangalia matendo yanayoadhimishwa kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, kama kielelezo cha faraja na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kila binadamu. Bikira Maria anasema Baba Mtakatifu Francisko ni sababu ya furaha ya waamini, anayewasaidia kuondokana na utumwa wa maisha ndani na nje ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana aliwapongeza watoto, familia na vyama vya kitume vilivyokuwa vimekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa ajili ya kubariki Sanam za Mtoto Yesu, zitakazowekwa kwenye mapango yaliyoandaliwa kwenye familia na parokia. Amewatakia heri na baraka tele katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na kwamba, wanaposali mbele ya Pango la Mtoto Yesu, wamkumbuke hata yeye katika sala zao.

Ni muhimu sana ikiwa kama wanafamilia watapata nafasi ya kujitenga na mambo ya dunia, ili kupata muda wa kusali. Ndiyo maana Baba Mtakatifu ameamua kuwazawadia waamini na watu wote wenye mapenzi mema waliofika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 14 Desemba 2014, kuwapatia zawadi ya kitabu cha sala kwa ajili ya matukio mbali mbali ya maisha, ili kuitakatifuza siku kwa kuzungumza na Mwenyezi Mungu, ili kweli furaha ya Yesu iweze kupata makazi yake kati ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko amelipongeza Kanisa nchini Poland wanapoadhimisha Mwaka wa Upendo, kama kielelezo cha mshikamano wa kidugu kwa kuwasha mishumaa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.