Tafuteni furaha ya kweli katika: Sala, Neno la Mungu na katika Matendo ya Huruma!
Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio ni mwaliko kwa Wakristo kushuhudia furaha
inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo; furaha ambayo inapaswa kumwilishwa kila
siku katika maisha ya Mkristo, kwani hii ni furaha inayomkirimia mwamini: utulivu
wa ndani na amani ya kudumu, hata pale anapokumbana na vizingiti vya maisha, kwani
amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayomwajibisha binadamu.
Mtakatifu
Paulo anawaalika Wakristo kuwa daima ni watu wa furaha kwa kusali ili kuomba, kushukuru,
kutukuza na kusifu. Wakristo watambue kwamba, wanatumwa kuwatangazia Watu wa Mataifa
Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.
Wakristo wamepakwa
mafuta ili kuwahubiri wanyenyekevu Habari Njema; kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia
mateka uhuru wao na wafungwa kufunguliwa kwao pamoja na kutangaza Mwaka wa Bwana.
Huu ndio wito ambao Wakristo wanapaswa kuufanyia kazi, ili kuwamegea wengine furaha
inayobubujika kutoka kwa Kristo!
Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni wakati alipofanya hija ya kichungaji kwenye
Parokia ya Mtakatifu Yosefu iliyoko Aurelio, Jimbo kuu la Roma. Anasema, furaha ya
Mkristo ijikite katika: Sala na Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kumwilisha ujumbe
huu katika matendo ya huruma. Waamini wajenge utamaduni wa kumshukuru Mungu kwani
amewajalia zawadi kubwa ya imani, wanayopaswa kuwashirikisha wengine kwa njia ya ushuhuda
wa maisha yao.
Baba Mtakatifu mwishoni mwa hija yake ya kichungaji Parokiani
hapo amekutana na kusalimiana na wananchi wanaoishi katika mazingira magumu, ili kuwatia
moyo wasikate tamaa!