Neno la Papa Francisko kwa makundi mbali mbali ya waamini!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 14 Desemba 2014 ametembelea Parokia ya Mtakatifu
Yosefu iliyoko Aurelio, Jimbo kuu la Roma na kupata nafasi ya kuzungumza pamoja na
makundi ya wanaparokia hii. Akizungumza na watoto, Baba Mtakatifu amewaambia kwamba,
mwaka huu ameadhimisha miaka 70 tangu alipopokea Komunio Takatifu kwa mara ya kwanza
kunako tarehe 8 Oktoba 1944.
Watoto waliokuwa wanajiandaa kupokea Ekaristi
Takatifu walitakiwa kuonesha heshima, adabu na ibada. Tarehe hiyo hiyo, jioni, waliimarishwa
kwa Sakramenti ya Kipaimara, changamoto kwa watoto wote watakaopokea Ekaristi Takatifu
na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kuikumbuka siku hii muhimu sana katika
maisha yao ya Kikristo! Hii ni siku ya kwanza ambayo Yesu ameingia rohoni mwao, ili
kuwa chakula chao cha maisha ya kiroho, kwa kuwajalia nguvu.
Baba Mtakatifu
anawataka Wakristo kuwakumbuka, kuwasaidia na kuwaombea Makatekista wanaojitaabisha
kwa ajili ya kuwarithisha imani. Waamini wafanye kumbu kumbu ya matukio haya kwa kujiandaa
kikamilifu katika maisha ya kiroho, yaani kwa kuungamana na kupokea Ekaristi Takatifu.
Baba
Mtakatifu akizungumza na watu wasiokuwa na makazi maalum, amewatakia kheri, amani,
baraka na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo, ili iwawezeshe kusonga mbele kwa
imani na matumaini, bila kukata tamaa, kwani iko siku Mwenyezi Mungu atawatembelea
katika maisha yao. Amewapongeza wote wanaojibidisha kujifunza amani kuendeleza juhudi
hizi kwani, Mwenyezi Mungu atawakirimia matunda ya amani kwa wakati muafaka.
Baba
Mtakatifu Francisko akizungumza na wagonjwa, amewaombea amani na faraja na kuwataka
kuendelea kusali kwa ajili ya Kanisa kwani wao ni chombo muhimu sana katika maisha
na utume wa Kanisa. Wagonjwa wapokee hali yao kwa imani, matumaini na uvumilivu, wakionesha
furaha na amani ya ndani.
Baba Mtakatifu amebahatika pia kuzungumza na Watoto
ambao wamebatizwa katika kipindi cha mwaka huu; watoto ambao walikuwa wameandamana
na wazazi pamoja na walezi wao. Amewataka wazazi kuwalea na kuwatunza watoto wao vyema
kwani hawa ni matumaini ya Kanisa na Jamii kwa ujumla. Watoto walirithishwe imani,
matumaini na mapendo; kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Siku ya Ubatizo, waamini wanapata
neema ya utakaso wanayopaswa kuitunza kwa njia ya maisha adili na safi.
Mwishoni,
Baba Mtakatifu amewaombea watoto hawa furaha, imani na matumaini ya kweli! Baba Mtakatifu
anasema, mtoto anapolia Kanisani, hii sehemu nzuri sana ya mahubiri na hapendi kuwaona
watu wakiwatoa mama zao nje, ili waweze kuwanyamazisha!