Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki la Bunda, Jumapili tarehe 14 Desemba 2014
ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Jumuiya ya Wanafunzi Watanzania Wakatoliki
wanaosoma na kuishi mjini Roma. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Parokia ya Mwili na
Damu ya Kristo, Roma, kwa ajili ya kuombea: haki, amani, upendo na mshikamano wakati
huu Tanzania inapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 53 tangu ilipojipatia uhuru wake
wa bendera kutoka kwa Mwingereza.
Askofu Nkwande
amewataka watanzania wanaosoma na kufanya shughuli zao mbali mbali nchini Italia,
kuwa ni cheche za furaha, matumaini na imani, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa
kwa ajili ya ujio wa Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Katika ulimwengu wa utandawazi
na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambao unaonesha dalili za kutaka kumweka Mwenyezi
Mungu pembezoni mwa mipango na mikakati yao ya maisha, kwa waamini wahakikishe kwamba,
Mungu anapewa kipaumbele cha kwanza kabisa, ili aweze kufanya maajabu katika maisha
ya mwanadamu.
Askofu Nkwande amewataka waamini kunyoosha mapito na maisha
yao, ili Masiha aweze kuzaliwa mahali pa salama na hatimaye, kuwawezesha kupata maisha
ya uzima wa milele. Jumuiya ya Watanzania inayoishi na kufanya utume wake mjini Roma,
imekumbushwa kwa namna ya pekee, kwa kweli ni mashhuhuda wa: imani, ukweli na haki,
mambo yanayohitaji ujasiri na nguvu kutoka kwa Roho Mtakatifu, ili Injili iweze kupenya
katika maisha na vipaumbele vya watu.
Ni Roho Mtakatifu anayewaongoza, anayewaelekeza
na kuwaimarisha tayari kutoka kifua mbele ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kama
alivyofanya Yohane Mbatizaji anayesimuliwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili
ya tatu ya Kipindi cha Majilio. Yesu Kristo akiwa amejazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu
aliweza kushuhudia upendo, huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwasamehe
watu dhambi zao; kwa kuwaponya magonjwa na madhaifu yao ya kimwili pamoja na kuwapatia
mahitaji yao msingi.
Askofu Nkwande anasema, Roho Mtakatifu anawajalia waamini
nguvu, ujasiri na neema ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa kutambua kwamba,
shida na magumu yataambatana nao hadi ukamilifu wa dahali. Waamini wanatakiwa kuwa
na ujasiri wa kutangaza Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ujasiri wa kushuhudia
kanuni maadili na utu wema, dhidi mielekeo potofu ya kijamii inayotaka kuhalalisha
hata mambo machafu kama ushoga kuwa eti ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Matendo
kama haya ni kutaka kujenga na kuimarisha urafiki na Shetani.
Askofu Nkwande
anawataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwavisha vazi la haki, huruma, mapendo
na ujasiri ili kupambana na kinzani za kimaadili, kama walivyofanya Mababa wa Kanisa
la Mwanzo, kiasi hata wakawa tayari kujisadaka maisha yao kwa ajili ya sifa na utukufu
wa Mwenyezi Mungu. Umefika wakati kwa Kanisa la Bara la Afrika kusimama kidete, kulinda
na kutetea tunu bora za Kiinjili bila ya kuyumbishwa.
Waamini kwa njia ya
ushuhuda wa maisha na matendo yao, wawafundishe watu namna ya kuambatana na Mwenyezi
Mungu; kwa kujikita katika kanuni maadili na ukweli; mambo msingi katika kuleta mabadiliko
katika maisha ya watu wanaotaka kukengeuka na kumezwa na malimwengu. Waamini wachangie
kwa hali na mali katika mchakato wa Uinjilishaji, kwa kulinda na kutetea hadhi, utu
na heshima ya binadamu; kwa kutumia hekima na busara.
Imeandikwa na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.