2014-12-15 08:44:04

Mshikamano wa dhati kutoka kwa Papa Francisko kwa wagonjwa wa Ebola!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, kuanzia tarehe 16 Desemba, 2014 anafanya hija ya upendo na mshikamano kwa wananchi wa Sierra Leone na tarehe 18 Desemba 2014 anatarajiwa kuwa nchini Liberia, mataifa ambayo yameathirika vibaya sana kutokana na kukumbwa kwa janga la Ebola!

Takwimu za Shirika la Afya Duniani, WHO, zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu 18, 000 ambao wameambukizwa Virusi vya Ebola. Zaidi ya wagonjwa 6, 500 wamekwishafariki dunia kutokana na ugonjwa huu huko Afrika Magharibi. Hija hii ya mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, inapania kuwatia shime na matumaini wadau wote ambao wanaendelea kupambana na ugonjwa huu wa hatari pasi na kukata tamaa.

Kardinali Peter Turkson katika hija hii anaambatana na Monsinyo Robert J. Vitillo, Mshauri mkuu wa masuala ya afya kutoka Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis. Kanisa Katoliki Afrika Magharibi ni kati ya wadau wakuu ambao wameendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola ambao umesababisha pia athari kubwa katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kuna kundi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kutokana na kuondokewa na wazazi pamoja na walezi wao.

Kardinali Turkson anasema, kuna haja ya kuisaidia mihimili ya shughuli za kichungaji Afrika Magharibi ili kuweza kutekeleza kikamilifu dhamana na utume wao kwa wagonjwa wa Ebola, kwa kuzingatia kanuni na mwongozo wa huduma kwa wagonjwa wa Ebola.

Baba Mtakatifu kwa nyakati mbali mbali ameonesha kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wagonjwa wa Ebola Afrika Magharibi, ndiyo maana wakati huu anapenda kumtuma Kardinali Peter Turkson, ili kuwatembelea watu walioathirika na ugonjwa wa Ebola, ili kuonesha mshikamano wake wa karibu. Anawashukuru na kuwapongeza wahudumu wa sekta ya afya wanaoendelea kutolea maisha yao kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi.All the contents on this site are copyrighted ©.