2014-12-15 12:21:04

Jubilee ya miaka 50 iwe ni changamoto ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi!


Shirika la Masista wa Kazi za Roho Mtakatifu linaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu lilipoanzishwa wakati huu ambapo Mama Kanisa anaadhimisha pia Mwaka wa Watawa Duniani. Askofu Isaac Amani Massawe wa Jimbo Katoliki Moshi, Jumatatu tarehe15 Desemba 2014 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya kilele cha Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Shirika hili lilipoanzishwa nchini Tanzania. RealAudioMP3

Askofu Joseph Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma anawaalika Masista hawa kufanya tafakari ya kina, ili miaka 50 iliyopita iwe ni fursa ya kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa wema na ukarimu wake katika maisha na utume wao kwa Watu wa Mungu Afrika Mashariki.

Jubilee hii anasema Askofu Mlola, iwe ni nafasi ya kuangalia maendeleo na changamoto wanazokabiliana nazo, huku wakidhamiria kuyapyaisha maisha na utume wao kwa Familia ya Mungu, kwanza kabisa kwa kubainisha utambulisho wao kama Wanashirika ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano, kama kielelezo makini cha ushuhuda makini wa maisha ya kitawa.

Askofu Joseph Mlola anawaombea Masista hawa neema na baraka kutoka kwa Roho Mtakatifu, ili azidi kuwaongoza, kuwaimarisha na kuwategemeza zaidi, ili waweze kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata na tamaa kwa changamoto na magumu mbali mbali wanayokutana nayo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.