Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo!
Tupo katika mwendelezo wetu wa kudadafua hati za mtanguso Mkuu wa pili wa Vaticani,
ili kuweza kuuleta ujumbe wake katika Kanisa la Nyumbani.
Leo tunalitazama
agizo la mababa wa Mtaguso liitwalo kwa lugha ya kilatini Unitatis Redintegratio,
inayohusu urudishaji wa umoja kati ya Wakristo. Mababa waliitazama historia ya Kanisa
la Kristo na kuona jinsi ambavyo kumekuwa na mimegeko katika vipindi mbalimbali vya
historia. Mimegeko na migawanyiko hiyo mababa wanaitazama kama makwazo makubwa kwa
ulimwengu na hivyo kufanya ulimwengu usiweze kuamini Injili ya Kristo.
Tumegawanyika
kana kwambwa Kristo aligawanyika! Tunasemanasemana, hatupendani wala kuheshimiana.
Na katika kutengana kwetu, wakati mwingine tunashambuliana kwa neno hilohio la Kristo.
Hayo ni makwazo kwa ulimwengu. Ni kama tumeukata mwili wa Kristo katika vipandevipande.
Kristo Yesu aliyetumwa na Baba tangu milele, kwa njia ya roho wake alipenda tuwe kitu
kimoja na ndiyo maana alisali akituombea umoja. Lakini katika ubinadamu wetu, tumekengeuka
matakwa hayo ya Kristo Yesu.
Mababa wa Mtaguso, wakisukumwa na dhamiri wajibifu
mbele za Mungu mmoja na wa Kweli, kwa njia ya hati hii wanatufundisha na kutuhimiza
sisi sote kujitahidi kujenga ushirikiano na wenzetu wengineo wanaomwamini Kristo.
Kurudisha umoja kati ya Wakristo wote kwa njia ya ushirikiano makini, ni moja ya malengo
ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Kwa njia ya Mtaguso huu, Mungu ametupatia
mwanga wa Uekumeni. Badala ya kusema turudi tuwe kitu kimoja, tunasema tushirikiane
katika umoja wa kweli huku tukiheshimu tofauti zetu. Yapo mambo ya msingi ambayo yanaweza
kutuweka katika meza moja. Kwa agizo la hati hii, Kanisa Katoliki linapaswa kushirikiana
na madhehebu yoyote ya Kikristo, ili kutoa mwanya zaidi kwa kazi ya Roho Mtakatifu.
Ni katika mtazamo huu, Kanisa Katoliki, linaona ishara chanya za kazi ya Roho Mtakatifu
na hata tunu za wokovu katika madhehebu mengine ya Kikristo.
Sura ya kwanza
inaeleza msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu Uekumeni. Mababa wanatufundisha kwamba
Kanisa ni moja tu, ambalo Kristo Bwana alilijenga juu ya mitume, nalo limekabidhiwa
kwa waandamizi wa mitume chini ya Warithi wa Mtume Petro (yaani Mababa Watakatifu).
Wakristo wa madhehebu mengine, ni Wakristo halisi, ijapo kuwa hawapo katika ushirika
kamili na sisi.
Mababa wanatualika tuwaheshimu, tushirikiane nao. Nao pia katika
imani yao, wanapiga mbio kumwelekea Mungu yuleyule mmoja na wa kweli. Makanisa yao
au jumuia zao vinatumiwa na Mungu kama vyombo vya wokovu, ila katika Kanisa Katoliki
tu unapatikana ukweli mzima na tunu zote za ukombozi. Hata hivyo tunakiri kwamba kwa
nafasi fulani, hatutumii vizuri neema hizo hata tunawakwaza wenzetu. Kwa fundisho
la hati hii, tulenge ukamilifu wa Kikristo ili Kanisa ling’ae mbele ya wote. Mbali
ya matendo ya kupendana ni muhimu pia kuwa na majadiliano ya kitaali-Mungu na mikutaniko
ya sala ya pamoja.
Sura ya pili inatuelekeza kuwa ni jukumu letu sisi sote
kutekeleza umoja huo kwa njia ya kurekebisha mapungufu ndani ya Kanisa, kuuambata
uongofu wa kweli, kusali, kushirikishana sakramenti, kufahamiana, kueleza imani kwa
ufasaha na bila kudharau madhehebu mengine, kushirikiana katika kutetea haki na amani
na kuleta maendeleo. Tushikamane kuukuza na kuulinda Ukristo wetu.
Mpendwa
msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, mimi na wewe ndio wadau wa kuleta
umoja wa Kikristo. Mababa wa Mtaguso wametuelekeza kuwa ni jukumu letu sisi sote.
Tunaleta ujumbe huu kwenye familia tukiamini kuwa watu wote, waungwana kwa wakorofi
wanatoka katika familia. Watoto wetu wakifundishwa imani ya kweli, hawatakuwa na sababu
ya kudharau Wakristo wa madhehebu mengine.
Ni aibu kubwa sana nyakati zetu
hizi sisi Wakristo tunapoanza kupigana vijembe majukwaani, kwa kunadi madhehebu yetu
kana kwamba ndiyo yana Kristo zaidi kuliko wengine. Hayo ni makwazo kwa ulimwengu.
Tukiwafundisha dini vizuri watoto wetu daima watajua thamani na wajibu wa kuilinda
imani ya baba zetu, imani ya kweli Katoliki, bila kukwaruzana na wengine.
Ni
mwito kwetu sote katika familia na katika ujirani, tuheshimiane, tupendane, na kwa
busara tushirikiane katika mambo ya imani zetu bila kuvuka mipaka yetu. Wale tunaowashambulia
Wakristo wenzetu kwa kejeli na vijembe kana kwamba wamepotea kabisa, hiyo ni dalili
wazi kuwa bado hatuijui dini yetu. Dini yetu sio ya watu wakorofi. Ni dini takatifu,
ya upendo na amani. Na wewe Mkatoliki huna haja ya kuanza kushambuliana na mtu anayekutuhumu
juu ya imani yako katika Ekaristi, Msalaba, Bikira Maria, Baba Mtakatifu nk. Hayo
hayawahusu. Kila mtu ale ugali kimyakimya upande wake.
Mkatoliki, ionee fahari
imani yako, tembea kifua mbele kwa sababu unamsadiki Kristo, Mwana wa Mungu aliye
hai. Ila, tunza kichwa! Sio lazima ujibu kila swali na kejeli unayoulizwa. Ila ujitahidi
sana, uifahamu imani yako vizuri, ili akitokea mtu anakuuliza kwa kutaka kuelewa,
mjibu na umfundishe kwa upole hadi aelewe. Ila mkejeli na mchokozi, mjibu kwa kukaa
kimya tu, na kumheshimu basi.
Ukiona mtu anadodosoadodosoa imani yako kwa
uchokozi huku amekufungia maspika-mzinga jukwaani, jua kuwa hana sera za dini yake.
Hao tuwaombee tu kimyakimya, bila kugombana. Sasa ikitokea wewe Mkatoliki, imani yako
huijui, ni mwigizaji, na anayekuchokoza naye hajui ya kwake, ni mfuata mkumbo tu,
halafu mnaingia katika mjadala wa mambo msiyoyajua, hapo lazima kutakuwa na kelele
nyingi tena kwa sauti kubwa zenye kuzaa matusi na mfarakano.
Kazi ya kulinda
umoja uliodhamiriwa na Kristo katika Kanisa, ni jukumu letu sote. Lakini hatutaweza
kwa nguvu zetu peke yetu. Hati hii inatuelekeza kuwa tunahitaji msaada wa Mungu mwenyewe.
Roho wa umoja atuangaze na kutuongoza. Wakati mwinginge, kazi ya kuleta umoja na ushirikiano
mwema inakwamishwa na midomo yetu na matumbo yetu. Wengi tunasahau lengo la Kristo,
badala yake tunaweka mbele ubinafsi wetu. Hapo tunakwamisha Injili ya Kristo! Ni katika
roho na sala na dhamiri njema tutaweza kufikia lengo wanalotuelekeza Mababa wa Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican
Kutoka katika Studio za Radio Vaticani, ni mimi Padre
Pambo Martin Mkorwe OSB