2014-12-15 14:58:38

Changamoto kwa wadau wa habari kutoka kwa Papa Francisko!


Wadau katika sekta ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kutekeleza dhamana hii kwa kuwajibika zaidi, kwa kujikita katika ukweli na uhuru; kwa kuijaza hadhira mambo msingi pamoja na kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Ni changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Kituo cha Televisheni cha TV 2000 kinachomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumatatu tarehe 15 Desemba 2014.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kwa bahati mbaya, mawasiliano ya jamii kwa kipindi kirefu yamejikita katika propaganda kwa ajili ya masuala ya kisiasa, uchumi na uthibiti wa teknolojia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba vyombo vya mawasiliano ya kijamii vinazungumza ukweli katika uhuru unaoheshimu na kuzingatia namna na mahali pa kuufikisha ukweli huu. Wanahabari wanapaswa kuasha tena uwezo wa watu kuwasiliana kikamilifu.

Vyombo vya mawasiliano viwe ni kichocheo kinachopania kuwajaza watu mambo msingi katika maisha, kwa kuwasaidia watu kufahamu kile kinachotangazwa, kwa kutoa nafasi kwa watu kufahamu mahudhui yanayokusudiwa badala ya kuwapatia watu majibu ya mkato. Baba Mtakatifu anasema haya ni mawasiliano ambayo yanafungua bila kufunga, kumbe, wanahabari hawana budi kumwachia nafasi Roho Mtakatifu afanye kazi ya kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano kati ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau wa habari kuhakikisha kwamba, wanazungumza na mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujiepusha na "dhambi za waandishi wa habari" zinazojikita katika kuwapaka watu matope; kueneza umbea na udaku pamoja na kutoa maamuzi katika ukweli wa mambo. Mawasiliano yasiwe ni kwa ajili ya "kumlipua mtu" au kuwajengea watu hofu! Mawasiliano ya namna hii yana walakini mkubwa.

Kumbe, kuna haja kwa wadau wa habari kuhakikisha kwamba, wanazungumza na mtu mzima: kiroho na kimwili; yote haya yanalenga pamoja na mambo mengine kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana katika ulimwengu mamboleo. Hapa watu wajifunze kutoa na kupokea kutoka kwa wengine.Baba Mtakatifu anawatakia kheri na baraka wafanyakazi wa Kituo cha Televisheni cha Baraza la Maaskofu Katoliki Italia wanapojipanga upya ili kutekeleza wajibu wao kikamilifu, ili kutoa huduma makini katika Kanisa.

Baba Mtakatifu anawashukuru kwa ushirikiano mzuri uliopo kati yao na Kituo cha Televisheni cha Vatican, ili kuhakikisha kwamba, Mafundisho ya Mababa wa Kanisa yanawafikia watu wengi zaidi. Anawashukuru wafanyakazi hawa kwa weledi na upendo wao kwa Injili anawatakia wote Noeli Njema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.