2014-12-15 09:04:59

Barua kutoka kwa Papa Francisko kwa ajili ya wafungwa!


Kipindi cha kutumikia adhabu gerezani ni fursa kwa mfungwa kukua ili hatimaye, aweze kupata amani na utulivu wa ndani na kwamba, kila mfungwa anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake. Kuna wafungwa wengi ambao wamemwandikia Baba Mtakatifu Francisko barua zinazoonesha mateso na mahangaiko yao gerezani, pamoja na kumshirikisha siri za maisha yao.

Si wakati wote Baba Mtakatifu amefaulu kuwajibu kwa wakati muafaka kutokana na sababu mbali mbali. Katika kipindi hiki cha Majilio, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia wafungwa wanaotumikia adhabu yao kwenye Gereza la Latina lililoko mjini Roma, barua ambayo imekabidhiwa kwa Padre Nicola Cupaiolo, Mhudumu wa maisha ya kiroho kwenye gereza hili, kwa lengo la kuwatakia kheri na baraka katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, Mwana wa Mungu anapozaliwa tena mioyoni mwa waamini.

Baba Mtakatifu anawaalika wafungwa wanapotekeleza adhabu yao, kuutumia vyema muda huu kama changamoto ya kukua na kukomaa, ili kuweza kupata amani na utulivu wa ndani, chemchemi ya maisha na matumaini mapya kutoka kwa Mwenyezi Mungu; matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya.

Anawapongeza wafungwa ambao wanatumia nafasi hii kufanya hija ya maisha ya kiroho, kwa kushirikiana na Padre Nicola Cupaiolo ambaye anawathamini na kuwaona kuwa ni ndugu na dada zake katika Kristo si tu kutokana na wajibu wa kiofisi.

Baba Mtakatifu anawaalika wafungwa kuendelea na hija hii ya maisha ya kiroho pasi na kukata tamaa na kwamba, anawashukuru wadau mbali mbali wanaoendelea kuwasaidia wafungwa katika mchakato wa kujiletea mabadiliko makubwa katika maisha. Baba Mtakatifu anapenda kuwazawadia Misale Mpya ya Altareni itakayowasaidia kugundua njia mpya ya maisha kwa kushikamana na Yesu Kristo katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Yesu ni mganga mahiri wa madonda na machungu yao ya ndani; ni rafiki mpendelevu anayeambatana nao katika maisha ya kila siku, kwa kuwapatia chakula kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya wokovu wao sanjari na nguvu ambayo haiwezi kuzuiwa na kuta za gereza.

Baba Mtakatifu Francisko anawaombea wafungwa ili waweze kufarijiwa na Kristo mwenyewe kwa kuwapatia amani na uwepo wake mwanana! Anasali kwa ajili yao binafsi, ndugu na jamaa bila kuwasahau wadau mbali mbali wanaotoa huduma gerezani hapo!

All the contents on this site are copyrighted ©.