2014-12-13 10:38:57

Papa akutana na Wakristo wa Syria mjini Vatican


Baba Mtakatifu ameonyesha ukaribu wake na kuwafariji Wakristo wengi wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi , hasa Syria na Iraq, ambako wanakabiliwa na unyama wa magaidi unao washinikiza Wakristo kuihama nchi yao. Papa ameonyesha hisia zake wakati akikutana na jumuiya ya Wakatoliki wa Syria ya Antokia , waliokusanyika hapa Roma, kwa ajili ya Mkutano wa Sinodi yao , ambayo imelazimika kufanyika nje ya nchi yao kutokana na uwepo wa vita na madhulumu mengi kwa jamii ya Wakristo nchini humo. Ujumbe huo ulikutana na Papa ukiongozwa na Patriaki Ignace Youssif III Younan, wa Kanisa Katoliki la Syria.

Kiini cha hotuba ya Papa kwa wageni wake hasa kililenga katika hatma ya jamii ya Kikristo Mashariki ya Kati. Alisema, kupitia kwao anaipaza sauti yake kwa jamii yao iliyotawanyikia duniani kote. Papa alitoa ujumbe wa kutia moyo, nguvu mpya ya kuishikilia imani yao , hasa kwa namna ya kipekee , Wakristo wa Iraki na Syria , daima waendelee kuweka tumaini lao kwa Bwana, wakati huu mgumu wa mateso na majaribu makubwa yanayowajengea hofu katika uso wa ghasia.

Sinodi Kanisa Katoliki la Syro, imefanyika kwa nia kuu ya kupata majibu katika mahitaji ya haraka ya kanisa, ambalo liko katika majaribu makubwa ya kiroho kwa waamini. Sinodi kwa namna ya kipekee, pia imefanya mchakato kwa ajili ya kufanya mageuzi katika Liturujia Takatifu , kama hatua mpya ya kuleta mwamko zaidi katika kupenda ibada. Kazi hii , Papa alisisitiza, inalazimu kuwa na tafakari za kina kwa ajili ya kupata utambuzi wa kutosha juu ya mila na desturi, kwa ufahamu kwamba, waamini wanajali unyeti wa zawadi ya Neno la Mungu ukuu wa Ekaristi.

Papa alionyesha kutambua hali ngumu katika Mashariki ya Kati, inayo sababisha na inaendelea kusababisha mabadiliko katika kanisa, waamini wake wengi , wakilazimika kwenda kuishi ugenini, hali inayotoa haja ya kuwa na mitazamo mipya ya kichungaji .

Papa amesema katika hali hiyo, mna changamoto mbili zilizofungamana. Kwa upande mmoja, ni kuwa aminifu katika asili yake; na kwa upande mwingine, ni kuwa na mchakato katika kazi za kichungaji kwenye mwingiliano wa asili ya tamaduni mbalimbali katika kukidhi huduma ya Kanisa na mazuri ya kawaida. Uhamaji huu wa waamini kuelekea mataifa mengine ni wazi hudhoofisha uwepo wa Wakristo Mashariki ya Kati, nchi ya manabii, wahubiri wa kwanza wa Injili na nchi ya mashahidi na watu wa Mungu wengi. Yote hayo alisisitiza Papa , yanahitaji uwepo wa Wachungaji na waamini jasiri, walio imara katika kushuhudia Injili kulingana na nyakati , jambo ambalo wakati mwingine si rahisi, kukabiliana na watu wa makabila tofauti na dini tofauti.

Papa aliendelea kuonyesha utambuzi kwamba, wengi wamekimbia na kutafuta hifadhi katika maeneo yaliyo salama zaidi , wamekimbia ukatili na unyama unaofanywa dhidi yao kwa sababu ya imani yao, wametoka katika nyumba zao bila ya kuwa na chochote hata kujua jinsi watakavyojikimu. Papa amewatia moyo kwamba wasikate tamaa Kanisa katika umoja wake kama mwili wa Bwana, linatembea nao katika mateso yao , kwa kujaribu kuratibu juhudi za kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu ya wote wale ambao kubaki nyumbani, wote wale waliokimbilia nchi nyingine.
Papa Francisco mwisho alihimiza Kanisa Katoliki Syria, liendelee na huduma yake kwa matumaini, huduma kwa jumuiya hii ya zamani ya Kikristo.
All the contents on this site are copyrighted ©.