Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Masita wa Kazi za Roho Mtakatifu,
nchini Tanzania!
Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu linaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu
lilipoanzishwa nchini Tanzania kwa kumshukuru Mungu aliyeliwezesha hadi sasa kuwa
na Masista 464 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika medani mbali mbali za maisha
ya mwanadamu. Shirika lina wasichana 105 ambao wako katika hatua mbali mbali za malezi,
tayari kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika maisha ya kitawa!
Shirika hili
linaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu lilipoanzishwa nchini Tanzania sanjari na
Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, unaowachangamotisha Watawa kushuhudia uzuri
wa kuacha yote kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani kwa njia ya kukumbatia Mashauri
ya Kiinjili; ili kutoa ushuhuda wa Kinabii unaojikita katika furaha ya kweli na ujasiri,
kwani watawa wanatambua kwamba, wanapendwa sana na Yesu.
Baba Mtakatifu Francisko
katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa anawachangamotisha watawa kujenga na kudumisha
umoja, upendo na mshikamano wa dhati katika maisha ya kijumuiya.
Katika mahojiano
maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, Sr. Eugenia Thomas, Mama Mkuu wa Shirika
la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu anagusia kwa ufupi karama ya Shirika lao; mahali
wanapotekeleza utume wao katika sekta ya elimu, afya, katekesi na huduma Parokiani.
Sr. Eugenia katika mahojiano haya anabainisha changamoto kubwa zilizoko mbele
yao ni pamoja na umaskini wa hali na kipato miongoni mwa watu wanaowahudumia; umuhimu
wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga umoja na mshikamano
wa kweli kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni watoto wa Mungu wanapaswa kuheshimiana,
kupendana, kuvumiliana na kusaidiana kwa ajili ya mafao ya wengi.
Sr. Eugenia
anasema wanawake ni vyombo vya amani na uti wa mgongo katika kuendeleza mchakato wa
maendeleo endelevu ya mwanadamu yanayogusa mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili.
Lakini wanawake wengi hasa Barani Afrika bado hawajawezeshwa kikamilifu ili kupambana
na mazingira na hivyo kuchangia zaidi katika kuziimarisha familia na jamii zao. Hii
ni changamoto kwa Kanisa kuendelea kuwajengea wanawake uwezo ili waweze kushiriki
kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.