2014-12-12 11:27:25

Ujumbe wa matumaini kwa Bara la Ulaya!


Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Tume ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Barani Ulaya anasema kwamba, hija ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Bunge la Ulaya, huko Strasbourg, Ufaransa hivi karibuni, imeonesha kutambua kwake kwa mafanikio makubwa yaliyokwisha kufikiwa katika mchakato unaopania kuziunganisha nchi za Ulaya katika umoja na mshikamano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii pamoja na kuwa na matumaini kwa siku za usoni.

Kuna baadhi ya wachunguzi wa mambo anasema Kardinali Marx walidhani kwamba, kwa vile Baba Mtakatifu si mwenyeji wa Ulaya hana uwelewa mkubwa wa masuala ya Bara la Ulaya, ikilinganishwa na watangulizi wake, lakini wengi wamepigwa na bumbuwazi, alipoipembua hali ya Ulaya kama "karanga" na kuwaacha wasikilizaji wake wakiwa wameduwaa!

Ni hotuba ambayo inaonesha wasi wasi, matumaini na dhamana ambayo Umoja wa Ulaya unaweza kutekeleza kwa ajili ya mustakabali wa wananchi wake pamoja na kuzingatia mafao ya wengi. Ulaya inaweza kuwa ni mahali pa rejea kutoka kwa watu mbali mbali duniani, kwa kuchangia kikamilifu katika mchakato wa maendeleo ya wengi, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kwa njia ya mikakati na utekelezaji wake katika ustawi na maendeleo ya watu, Bara la Ulaya linaweza kuwa ni mfano bora wa kuigwa.

Baba Mtakatifu amewakumbusha wanasiasa wa Bara la Ulaya kwamba, mwanadamu, utu na heshima yake pamoja na haki zake msingi ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa kuunganisha Nchi za Ulaya na kuwa ni kitovu cha sera na mikakati ya Umoja wa Ulaya, kwa kutambua kwamba, Kanisa limechangia kwa namna ya pekee katika ustawi na maendeleo ya Bara la Ulaya kwa kujikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, yanayomtambua binadamu kuwa ni kiumbe jamii, mwenye haki na nyajibu zake; ni kiumbe anayepaswa kushirikiana na wengine kwa ajili ya mafao ya wengi.

Mchakato mpya wa Bara la Ulaya hauna budi kujikita katika utu na heshima ya binadamu; kwa kutambua na kuheshimu utakatifu wa maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu badala ya kukazia masuala ya uchumi. Ulaya inapaswa kuangalia mbele kwa matumaini licha ya kinzani na changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa wakati huu.

Kardinali Reinhard Marx anasema kwamba, hija ya kikazi ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Bunge la Ulaya, umekuwa ni ujumbe wa matumaini kwa wananchi na Kanisa katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.