Mwanadamu apewe kipaumbele cha kwanza katika mikakati ya maendeleo!
Jumuiya ya Kimataifa tangu mwaka 2008 ilijiwekea mikakati ya kupambana na baa la umaskini
miongoni mwa watu, ili kufikia mwaka 2017, baa hili liweze kupewa kisogo na Jumuiya
ya Kimataifa kwa watu kuwa na maisha bora zaidi.
Ni katika
mwelekeo huu wa kupambana na vizingiti vinavyokwamisha maendeleo ya mwanadamu, Jumuiya
ya Kimataifa ikajiwekea Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015, mwaka
mmoja tu kuanzia sasa.
Takwimu zinaonesha kwamba, kumekuwepo na mafanikio
katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia, hata hivyo Jumuiya ya Kimataifa
haina budi kujifunga kibwebwe kwani bado kuna changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa
kazi, ili kuondokana kabisa na baa la umaskini wa hali na kipato duniani. Ili kweli
watu wengi waweze kupata mafanikio makubwa katika maisha, kuna haja ya kuwa na mikakati
makini ya maendeleo, matumizi bora na sahihi ya rasilimali, kuunganisha nguvu, kwa
kujikita katika kanuni ya auni kati ya mataifa; kuratibu na hatimaye, kupima maendeleo
yaliyokwisha fikiwa.
Mikakati ya maendeleo ijielekeze zaidi kwa kuangalia
uhalisia wa maisha ya watu husika kadiri ya mazingira yao; isikilize uzoefu wa watu
husika na kutoa majibu muafaka kwa kusoma alama za nyakati bila mizengwe ya kisiasa
ambayo wakati mwingine imekwamisha mchakato wa maendeleo endelevu miongoni mwa watu.
Ni
mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa Vatican
kwenye Umoja wa Mataifa katika mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lililokuwa
linajadili kuhusu maendeleo. Mikakati ya kupambana na umaskini ijielekeze zaidi katika
sera zinazodumisha mshikamano, ushirikishwaji wa watu pamoja na kutoa fursa za ajira
kwa watu kumudu gharama za maisha.
Pengo kati ya maskini na matajiri ni changamoto
kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi, ili kukuza na kudumisha amani na utulivu kati ya
jamii, kwani kinzani na migogoro mingi kwa sasa ni matokeo ya kundi kubwa la maskini
kuendelea kuogelea katika umaskini wa hali na kipato na watu wachache kuendelea kufaidika
na rasilimali na utajiri wa nchi. Kutokana na hali kama hii, utu na heshima ya binadamu
vinawekwa rehani. Wanawake washirikishwe katika kuibua, kupanga na kutekeleza mikakati
ya maendeleo katika nchi zao na kwamba, huduma ya elimu, afya na maendeleo, itolewe
bila ubaguzi.
Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu, unapongeza nchi wanachama
wa Umoja wa Mataifa ambazo zimefanikiwa kupunguza tofauti za usawa wa kijinsia kwa
kusema kwamba, bado kuna kazi kubwa inayopaswa kutendwa, ili kweli wanawake waweze
kushirikishwa kikamilifu katika masuala yanayohusu mikakati ya maendeleo na maboresho
ya maisha. Ikumbukwe kwamba, umaskini unaweza kujionesha katika medani mbali mbali
za maisha na wala si tu kwa mtu kukosa fedha.
Mikakati ya maendeleo inapaswa
kumlenga mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuwekeza katika matumizi bora ya rasilimali
na utajiri wa nchi, ili kusaidia mchakato wa kuleta maboresho ya maisha ya watu wengi
zaidi. Lengo la Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na baa la umaskini awe ni binadamu
na mahitaji yake msingi na wala si maendeleo ya vitu, huu ndio mshikamano wa kweli
unaopaswa kuoneshwa na Jumuiya ya Kimataifa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.