2014-12-12 14:38:55

Mtandao mpya wa Radio Vatican!


Radio Vatican iliyoanzishwa kunako tarehe 12 Februari 1931, inaendelea kusoma alama za nyakati, ili kwenda sanjari na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, kwa kuhakikisha kwamba, "inakula sahani moja na wasikilizaji, wasomaji na watazamaji wake" kwa kutumia mitandao ya mawasiliano ya kijamii.

Ni Radio inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican ambayo inapenda kujielekeza zaidi katika kuhabarisha walimwengu kuhusu maisha na utume wa Baba Mtakatifu; mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaotekelezwa na Mama Kanisa katika maisha ya watu: kiroho na kimwili; masuala ya Jumuiya ya Kimataifa; majadiliano ya kidini na kiekumene; muziki na mambo mengi ambayo kimsingi ni sabuni ya roho kwa wasikilizaji wengi!

Utajiri wote huu unapatikana katika lugha arobaini zinazotumiwa na Radio Vatican kurusha matangazo yake sehemu mbali mbali za dunia; Lugha ya Kiswahili, ikipewa kipaumbele cha pekee kwa Bara la Afrika. Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria wa Guadalupe, uongozi wa Radio vatican umezindua mtandao mpya wa Radio Vatican unaojitahidi kusoma alama za nyakati katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi, huko walikojichimbia, lakini wana kiu ya kutaka kusikia kile kinachoendelea katika maisha na utume wa Kanisa.

Mtandao mpya wa Radio Vatican ambao umefanyiwa maboresho makubwa kwa sasa utapatikana katika lugha 37 kufuatana na mpangilio wa Alfabeti, lengo ni kuiwezesha Radio Vatican kuendeleza mchakato wa majadiliano kwa kutumia mitandao ya kijamii, utume unaotekelezwa kwa kushirikiana pia na Kituo cha Televisheni cha Vatican kinachotoa picha za matukio makuu yanayofanywa na Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake.

Kwa njia ya teknolojia ya mawasiliano, watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaweza kufuatilia matukio kwa lugha mbali mbali kutoka katika mtandao wa Radio Vatican na kwa matukio makuu, Radio Vatican pia inaendesha programu za moja kwa moja katika baadhi ya lugha. Takwimu zinaonesha kwamba, watumiaji wa mtandao wa Radio Vatican wamegawanyika kama ifuatavyo:

Ulaya watumiaji wa mtandao wa Radio Vatican ni asilimia 57%
Bara la Amerika ni asilimia 29.14%
Bara la Asia na Oceania ni asilimia 11.22%
Bara la Afrika ni asilimia 2.50%.

Watumiaji wa mtandao wa Radio Vatican kwa kufuatia jinsia wamegawanyika kama ifuatavyo: Wanawake ni asilimia 46% na wanaume ni asilimia 54%. Jambo la kufurahisha ni kuona kwamba, watumiaji wengi wa mtandao wa Radio Vatican ni vijana wenye umri chini ya miaka 35. Radio Vatican, mkongwe katika mawasiliano ya jamii, inaendelea kusoma alama za nyakati kwa kuhakikisha kwamba, inatekeleza dhamana na wajibu wake mintarafu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari kwa watu wa kizazi kipya.

Lengo ni kuendeleza mchakato wa mawasiliano na kuliwezesha Kanisa kukuza na kudumisha majadiliano katika maisha na utume wake kwa njia ya matumizi ya mitandao ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.