2014-12-12 07:23:37

Makardinali wapya kutangazwa na kusimikwa tarehe 14-15 Februari 2015


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwatangaza na kuwasimika Makardinali wapya pamoja na kufanya mkutano wa Makardinali wote kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 15 Februari 2015. Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Baba Mtakatifu kuteuwa Makardinali, tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.

Ni maneno yaliyosemwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Alhamisi tarehe 11 Desemba kufuatia mkutano wa Baraza la Makardinali washauri, uliofanyika kwa muda wa siku tatu na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko aliyeshiriki kwa makini kwa kusikiliza na kuchangia maoni yake. Baraza la Makardinali washauri litafanya tena mkutano wake kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 13 Februari 2015 na baadaye Makardinali wote watashiriki katika mkutano huu, ili kujadili kwa kina na mapana kuhusu mchakato wa mageuzi ya Sekretarieti ya Vatican.

Baraza la Makardinali limepata nafasi ya kusikiliza taarifa iliyotolewa na Askofu Marcello Semeraro, Katibu wa Baraza la Makardinali, kufuatia, maoni, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na wakuu wa Sekretarieti ya Vatican chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 24 Novemba 2014. Makardinali wamepembua kwa kina na mapana ushauri na mapendekezo yanayotaka kuleta mabadiliko katika Mabaraza mawili ya Kipapa: kwa kuunganisha: Baraza la Kipapa la Walei na Baraza la Kipapa la Familia; kuunda Baraza la Kipapa la haki, amani na mapendo. Huu ni mchakato ambao bado unaendelea kufanyiwa kazi na hakuna maamuzi thabiti ambayo yamekwisha kutolewa hadi sasa.

Tume ya Kipapa ya kusimamia watoto wadogo inayoongozwa na Kardinali Sean Patrick O'Malley imetoa taarifa yake na kwamba, inatarajia kufanya mkutano wake wa mwaka kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 8 Februari 2015 kwa kuwashirikisha wajumbe wapya watakaokuwa wameteuliwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Idadi hii itaongezeka kutoka wajumbe tisa hadi kufikia wajumbe kumi na nane, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Padre Federico Lombardi.

Katika mkutano huu, Bwana Joseph F.X Zara, makamu mratibu wa Baraza la Kipapa la Uchumi, ameshiriki pia kwa kuchangia kwa kina na mapana mabadiliko ya kiuchumi yanayofanywa kwa sasa mjini Vatican ili kuongeza tija na ufanisi zaidi, kwa kuzingatia ukweli, uwazi na uwajibikaji. Kwa sasa Baraza hili linaendelea kuandika Katiba na mwongozo wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.