2014-12-11 07:51:58

Watoto kutoka Parokia za Jimbo kuu la Roma kufurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili ijayo!


Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio, tarehe 14 Desemba 2014, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya watoto, wazazi na walezi wao kutoka katika Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma. Haya ni mapokeo ambayo yamekuwepo kwa takribani miaka arobaini iliyopita.

Baada ya maadhimisho haya, watoto watakusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ili kupata baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Sanamu za Mtoto Yesu zitakazowekwa kwenye mapango yaliyoandaliwa kwenye: Familia na Parokia. Maadhimisho haya katika Kipindi hiki cha Majilio yanaongozwa na kauli mbiu "Furaha i pamoja nasi". Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio, itakuwa ni siku ya furaha kwa watoto na wazazi wao, furaha ambayo wanataka kumshirikisha Baba Mtakatifu Francisko.

Watoto hawa watashiriki kikamilifu kwenye Sala ya Malaika wa Bwana, ili baadaye, waweze kupeleka furaha hii katika familia zao, kwa kuzingatia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anapenda waamini kutoa kipaumbele cha kwanza katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, wakati huu, Kanisa linapojiandaa kwa ajili ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, inayoongozwa na kauli mbiu "Wito na utume wa familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo".All the contents on this site are copyrighted ©.