Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi inasema kwa sasa Malawi
inakabiliwa na ukata mkubwa kutokana na ukweli kwamba, wafadhili mbali mbali waliokuwa
wanachangia katika bajeti ya Serikali wamejitoa kutokana na ufisadi na ubadhirifu
wa mali ya umma. Tume ya haki na amani inasema, kwa hakika Malawi bado inahitaji kupata
misaada kutoka kwa wafadhili, vinginevyo watu wengi wataendelea kuteseka sana.
Jambo
la msingi ni wadau kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba, fedha inayotolewa
inawafikia walengwa pamoja na kuwawajibisha kisheria watu waliokwapua mamillioni ya
dolla za kimarekani kwa ajili ya mafao yao binafsi, ili wawe fundisho kwa watu wenye
tabia chafu inayodidimiza mchakato wa maendeleo na mafao ya wengi nchini Malawi.
Katika
miaka ya hivi karibuni ubora wa huduma ya afya, elimu na maji umeendelea kudidimia
kwa kiasi kikubwa kiasi cha kuhatarisha usalama na maisha ya wananchi wa Malawi. Baadhi
ya huduma zimeanza kutolewa na Makampuni ya watu binafsi, jambo ambalo si rahisi kwa
wananchi wengi wa Malawi kuchangia katika huduma hizi. Wananchi wa Malawi wameanza
kuwawajibisha viongozi na wafanyakazi wa umma wanaoonesha tabia ya wizi na ufisadi
wa fedha na mali ya umma, kwani wamechoshwa kuona watu wakimezwa na uchu wa mali!