2014-12-11 10:40:23

Uchaguzi mkuu kisiwe ni kikwazo cha maendeleo ya demokrasia nchini Burundi


Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi katika ujumbe wake kwa waamini na watu wote nchini humo katika kipindi hiki wanapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Burundi kunako mwaka 2015, wanapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wananchi ambao kwa njia ya kupiga kura wanafanya mabadiliko katika Serikali kwa kuwachagua viongozi wanaowataka.

Hii ni sehemu ya utekelezaji wa haki yao msingi Kikatiba pamoja na kudumisha msingi wa demokrasia na maendeleo ya kweli! Kanisa linathamini mfumo wa demokrasia kwa sababu unawahakikishia wananchi ushiriki wao katika maamuzi ya kisiasa, uwezekano wa kuchagua na kuwawajibisha viongozi wao sanjari na kuwabadilisha kwa njia ya amani wakati unapowadia.

Demokrasia ya kweli inawezekana tu pale Serikali inapotawala kwa kuzingatia sheria, utu na heshima ya binadamu. Uchaguzi ni wajibu na haki ya kila mwananchi kwa mujibu wa sheria sanjari na kupima mafanikio, matatizo na changamoto zilizojitokeza katika uongozi uliopita.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawapongeza wananchi kwa ukomavu wa kisiasa unaojionesha kwa njia ya ushiriki wa kupiga kura kwani hadi sasa hakuna mtu ambaye amesusia kushiriki katika uchaguzi mkuu kadiri ulivyopangwa na vyama vya kisiasa. Maaskofu wanasema, kwa sasa kuna hali ambazo zinatishia majadiliano ya kisiasa, mbinu na mikakati ya uchaguzi kuelemea upande mmoja tu, jambo ambalo linaweza kuwa ni hatari kubwa kwa mustakabali, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Wananchi wa Burundi wanajiandaa kushiriki katika mchakato wa upigaji kura, huku amani na usalama wa wananchi viko mashakani. Kuna makundi ya watu yanayoteka watu nyara na kuwapora; yanayoua bila huruma pamoja na kuendelea kufanya uhalifu pamoja na kutumia lugha ambayo inachochea uvunjifu wa amani na usalama. Inaonekana kana kwamba, kuna vijana ambao wako tayari kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kufanya vurugu nchini Burundi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi, linawataka wananchi wote wa Burundi katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanawajibika barabara katika maamuzi na matendo yao, ili kweli uchaguzi mkuu nchini humo uweze kuwa huru, kweli na wazi; uchaguzi unaozingatia sheria na demokrasia ya kweli. Uchaguzi mkuu usiwe ni kikwazo cha maendeleo ya demokrasia nchini Burundi, bali chachu ya kujenga na kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.