Mara nyingi tunasikia toka vyombo vya habari kwamba kuna watu wanashikiliwa na Polisi
kwa uhalifu na wengine wamekamatwa ili kuisaidia vyombo vya dola kufanya upelelezi.
Mashahidi wa mahakamani wanategemewa kutoa ushuhuda jinsi kituko au uhalifu ulivyotokea.
Kutokana na makashkash za mahakamani watu wengi wanatoroka kuweko sehemu za
tukio wasije wakashikwa kuwa mashahidi. Hebu leo tumfuatilie jamaa mmoja aliyeshikiliwa
na Mungu ili atoe ushuhuda wa kituko kimoja kilichojili hapa duniani. Tunaambiwa kuwa,
“Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda.”
Yohane ndiye mtu huyo aliyeshikiliwa na Mungu kwa malengo ya kutoa ushuhudia.
Yohane mwenyewe alijua ni kwa malengo aliyotumwa kufanya hapa duniani na alitambua
makashkash yanayoweza kumjiri kutokana na kuwa shahidi. Maana ya jina la mtoa ushuhudi
linashuhudia ni kitu gani, amekuja kushuhudia, kwa sababu kila jina linatakiwa kuitambulisha
hadhi ya mtu.
Jina hili Yohane linatokana na lugha ya kihebrania Yohanan lenye
maana ya “Mungu ni upendo.” Hivi mbatizaji amezaliwa duniani kwa malengo
ya kuushuhudia upendo. Injili nyingine zinamchora Yohane kuwa ni mtangulizi, anayeandaa
ujio wa masiha, anawaandaa watu kusubiri kule kutekelezeka kwa unabii wa Agano la
Kale, hasa namna ya kumpokea masiha. Kumbe mwinjili Yohane anamwonesha Yohane Mbatizaji
kama shuhuda, yaani mtu anayeshuhudia.
Hiyo ndiyo hatua ya kwanza na katika
hatua hii tunaweza kuanza kujiuliza: “Mimi ni nani na nimetumwa hapa duniani kwa ushuhuda
gani, na niushuhudie vipi uwepo wangu. Kadhalika yatakiwa nijihoji ninaitwa jina gani
ambalo Mungu anaweza kulifahamu. Mungu ni upendo na analinganishwa na Mwanga au nuru
ambayo Yohane aliishuhudia. “Yohane alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru,
wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile
nuru.” Mwanga ni kitu kizuri hata jicho linapenda kuuona mwanga na kilikuwa kitu cha
kwamza kuumbwa.
Kuona mwanga maana yake kuzaliwa, kadhalika ni alama ya uzima.
Watu wanapoamkiana wanajibu “Tupo bado tunaona mwanga au kumekucha”. Mbatizaji anao
utume muhimu, na mara tatu yasema kwamba amekuja kuushuhudia mwanga. Yohane anatolea
ushuhuda mwanga huo mbele ya watu wenye mamlaka, mbele ya wanafunzi wake na mbele
ya watu wote.
Yesu akiwa kama mtu mwenye umbo la kibinadamu alikuwa anaonekana
na kila mtu, uso wake haukufichika na watu wote walikuwa wanauona. Katika mtazamo
wa kawaida, tungeweza kusema kuwa Mbatizaji alikuwa anaona kitu kile ambacho watu
wote walikuwa wanakiona kwa macho yao ya kawaida. Kwa hivyo, kama Yesu ni Nuru basi
watu wote waliweza kuiona Nuru hiyo lakini hawakuitambua. Kumbe Yohane Mbatizaji alikuwa
anamtazamo mwingine wa mambo, kutokana na uwezo aliopewa na Roho na mwanga wa Mungu
aliweza kuona zaidi ya pale wanapofikia kuona wengine kwa macho yao ya kawaida, kama
ilivyoandikwa “Wenye heri wale wanaoona kile mnachoweza kukiona ninyi.”
Vivyo
hivyo, tunaweza kusema juu ya maisha yote ya Yesu hata ujumbe aliotoa, siyo wote walibahatika
kuutambua. Ingawaje Yesu alifanya mambo yake hadharani bila mficho, watu wengi walishuhudia
lakini walitoka mbukwa, kwani waliyaona kwa jicho la kiyakinifu, yaani kwa macho ya
kawaida.
Tungeweza kusema kwamba Yohane Mbatizaji aliyekuwa kwenye tukio,
akaishuhudia hiyo nuru kwa jicho la roho. Na akawa tayari kutumwa kutekeleza kazi
ya kuishuhudia nuru hiyo. Huo ndio mwito tunaoalikwa kuushuhudia sisi, kwanza namna
ya kuiona hiyo nuru kama alivyoona mbatizaji. Kwamba Mungu ni upendo na upendo huo
unauona katika Kristo.
Kisha kuna ujumbe uliotumwa na viongozi wa Yerusalemu
waliofika kumwuliza Yohane ni nani. Yohane alijulikana sana nchini pengine kumpita
hata Yesu. Haiba ya Yohane iliweza kumtisha hata Herode Antipa, aliyeogopa kwamba
Mbatizaji angeweza kuhamasisha watu kufanya hata mgomo au mapinduzi fulani na watu
wangemsikiliza. Kadhalika watu wa dini – makuhani – walikuwa na wasiwasi naye kwa
sababu, wengine walimdhani kuwa labda ndiye Masiha mwenyewe.
Kama anavyosema
nabii Malakia kwamba Masiha ajaye angeisafisha dini na kuiweka sawa hasa kulitakasa
hekalu, kwani humo kulikuwa kunatendeka madhambi mengi. Ndani ya hekalu kulikuwa na
utapeli, rushwa ilikithiri hadi kufikia kiasi cha kupanga duka la kubadilisha pesa
na biashara ndogondogo ndani ya Hekalu.
Hivi hata nao waliogopa, wakaenda
kumwuliza: “Wewe ni nani?” Lakini yeye anaungama na kushuhudia waziwazi kwamba: “Mimi
siyo Kristo”. Hapa hata sisi tunaweza kujiuliza je, tuna hadhi na nafasi gani, ili
tusiweze kukosea kushuhudia wito na utume wetu. Tusije tukachukuliwa na upepo tukapitiwa
na kushindwa kushuhudia utu wetu. Tusijiachilie kutekwa na watu wenye wivu, watu wabaya,
bali tuongozwe na nuru ambayo ni Kristo. Wanaendelea kumwuliza “kama wewe siyo Masiha
basi ni nani? Je, ni nabii Eliya?” Mbatizaji anajibu kwamba siyo yeye. Kisha wanamwuliza
swali zuri linaloweza kuwa fundisho kwetu “Unasema nini juu ya wewe mwenyewe.” Maana
yake wewe ni nani? Unajifahamu vipi.
Hapa hutakiwi kutoa kitambulisho au kuonesha
uso wako, bali wewe mwenyewe unajishuhudiaje. Unajiju vipi? Yohane anajijua yeye ni
nani hivi anajibu: “Mimi ni sauti ya mtu anayeshuhudia huko jangwani.” Katika kipengee
hiki yaonekana maelezo sahihi yangeweza kuwa yale ya mt. Augustino pale anapotofautisha
kati ya sauti na neno.
Sauti ni ile inayosikika mtu anapoongea. Hiyo inadumu
kwa muda fulani halafu inapotea. Lakini sauti inaacha neno au ujumbe. Sauti yatakiwa
ififie na neno libaki. Sisi wabatizwa tuko hapa duniani kama sauti, inayoshuhudia
kwamba Yesu ni mwanga unaoangaza gizani. Hiyo ndiyo tabia tunayotakiwa kuwa nayo.
Kama tunaongea tu na kutoa sauti kuhubiri, juu ya mwanga bila kushuhudia kwa matendo
katika maisha yetu hapo sauti hiyo haiwakilishi ujumbe wowote ule bali inakuwa ni
“debe tupu haliachi kutika.”
Wanamwuliza tena “kwa nini basi unabatiza kama
wewe siyo Masiha?” Lakini yeye anajibu kwamba mimi ninabatiza kwa maji. Maana yake
ni alama inayopita inayomaanisha kuacha mambo ya kale ili kuanza maisha mapya. Ubatizo
wake ni wa kuwafanya watambue kwamba, wanaishi katika giza. Sisi leo hatupokei ubatizo
wa Yohane, lakini ni alama inayoweza kutufaa hata sisi leo.
Endapo uko gizani,
basi kumbuka kwamba inabidi ufanye mang’amuzi haya ya ubatizo yaani, kusikiliza ujumbe
wa Yohane na kufanya ubatizo wa mpito kutoka gizani na kuingia mwangani. Kisha Yohane
anaendelea kusema: “kati yenu kuna mwanga, na ambao hamuufahamu. Fungueni macho ya
kiroho muweze kumwona kwani nuru hiyo iko kati yetu. Iko kati ya watu wanaoifahamu
na wanaoiishi hiyo nuru, yaani watu wanaofaulu kuunganisha maisha yao na mwanga. Kwa
hiyo leo Yohane anatuandaa kujijua sisi ni nani, kuipokea nuru hiyo na kuishuhudia
katika maisha yetu.