Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu imechapisha Mwongozo wa Sinodi ya Kawaida ya Maaskofu
itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, kwa kuongozwa
na kauli mbiu "Wito na Utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo".
Mwongozo
wa Kazi, unaojulikana katika lugha ya Kilatini kama "Lineamenta" ni hati ya kwanza
kutolewa katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu na kwa namna ya pekee,
kama ilivyoelekezwa na Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kufunga rasmi maadhimisho
ya Sinodi maalum ya Maaskofu, iliyoadhimishwa mjini Vatican, mwezi Oktoba 2014. Mwongozo
huu unatokana na Hati ya Mababa wa Sinodi, "Relatio synodi" iliyotolewa wakati wa
maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu na kwa sasa imewekwa katika mfumo wa maswali,
ili kusaidia mchakato wa maandalizi ya hati ya pili, ijulikanayo kama Hati ya Kutendea
Kazi, "Instrumentum Laboris.
Hati hii imetumwa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
sehemu mbali mbali za dunia, kwa wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume na
kwa Sekretarieti ya Vatican. Lengo la Hati hii kuiwezesha Familia ya Mungu kuanza
kuchangia kwa kina na mapana hoja mbali mbali zitakazofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi
kuhusu familia.
Matunda ya kazi hii yatakusanywa na Sekretarieti ya Sinodi
za Maaskofu ili kuandaa Hati ya Kutendea Kazi, "Instrumetum Laboris". Ili kufanikisha
zoezi hili, majibu kutoka kwenye Mabaraza ya Maaskofu na wadau mbali mbali hayana
budi kuwa yameifikia Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu ifikapo tarehe 15 Aprili 2015,
tayari kuendelea na hatua nyingine zaidi.
Waamini wanaalikwa kwa mna ya pekee,
kuendelea kuwasindikiza Mababa wa Sinodi kwa njia ya sala na maadhimisho mbali mbali
yanayopania kutangaza Injili ya Familia kati ya Watu wa Mataifa. Sherehe ya Familia
Takatifu kwa Mwaka 2014 ipewe kipaumbele cha pekee na wanafamilia wote, ili kuonesha
umoja, upendo na mshikamano katika wito na maisha ya kifamilia.