Mahusiano kati ya Vatican, Kanisa na Serikali ya Msumbiji katika mchakato wa maendeleo
endelevu; haki, amani na upatanisho wa kitaifa; umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti
biashara ya silaha duniani ambayo imekuwa ni chanzo cha majanga makubwa kwa mataifa
mengi; umaskini na ukosefu wa usawa kati ya watu; ni kati ya mambo msingi ambayo Rais
Armando Emìlìo Guebuza wa Msumbiji pamoja na Baba Mtakatifu Francisko waligusia, walipokutana
hivi karibuni mjini Vatican.
Rais Guebuza alikutana na kuzungumza na Radio
Vatican anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwa namna ya pekee mchakato
wa kuendeleza amani, utulivu na upatanisho wa kitaifa kama kikolezo cha maendeleo
endelevu miongoni mwa wananchi wa Msumbiji ambao kwa miaka mingi wamejaribiwa na kuteseka
kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Baba Mtakatifu anawachangamotisha
wananchi wa Msumbiji kujifunga kibwebwe katika kupambana na umaskini wa hali na kipato,
kwa kujiwekea mikakati ya maendeleo endelevu inayogusa maisha ya mtu mzima: kiroho
na kimwili; mambo ambayo hayana budi kujikita katika umoja na mshikamano wa kitaifa.
Rais Guebuza anasema, Msumbiji kama taifa changa ambalo limejaribiwa sana
kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe bado halijawa na msingi thabiti wa umoja wa
kitaifa, mwaliko kwa wananchi wa Msumbiji kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano
wa kitaifa kwa kuheshimu tofauti zinazojitokeza kati yao na kwamba, tofauti hizi zisiwe
ni kizingiti cha umoja wa kitaifa.
Serikali ya Msumbiji licha ya changamoto
mbali mbali zilizopo, inaendelea kucharuka katika mikakati ya kuwaletea wananchi wake
maendeleo endelevu kwa kutumia kikamilifu rasilimali iliyopo kwa ajili ya mafao ya
wengi, ili kujenga uchumu imara zaidi. Kwa miaka mingi, Italia imekuwa ni mwekezaji
mkuu nchini Msumbiji na kwamba, imeonesha nia ya kuendelea kuwekeza zaidi na zaidi.
Kwa sasa Shirika la Nishati la Italia, ENI linaendelea kufanya upembuzi yakinifu ili
kuanza kuchimba gesiasilia ambayo inapatikana kwa wingi nchini Msumbiji.
Rais
mpya wa Msumbiji Bwana Filipe Nyusi, anatarajiwa kuapishwa wakati wowote mwanzoni
mwa mwezi Januari, 2015 baada ya kukamilisha mchakato wa kurithishana madaraka kadiri
ya sheria na kanuni za nchi. Kwa sasa anasema Rais Guebuza yeye ndiye nahodha wa Serikali
ya Msumbiji na kwamba, Rais mpya anatarajiwa kuendeleza mahusiano mema kati ya Msumbiji
na nchi marafiki na kwamba, ni kiongozi ambaye anapenda kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wake.
Bwana Nyusi ni kiongozi ambaye historia
ya Msumbiji iko kiganjani mwake ni mtu ambaye anapenda kukuza na kudumisha mahusiano
ya kirafiki na nchi jirani pamoja na zile zinazozungumza lugha ya Kireno.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.