Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika
ya Kati katika mahubiri yake wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa
Dhambi ya Asili, iliyofanyika tarehe 8 Desemba 2014, amewataka waamini na watu wote
wenye mapenzi mema nchini humo kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuanza kujikita katika
mchakato wa msamaha na upatanisho wa kitaifa kwa kuachana na matendo ambayo yanagumisha
ustawi na maendeleo ya watu!
Umefika wakati wa kuachana na mapambano ya silaha
ambayo yamekuwa ni janga la kitaifa tangu nchi hii ilipojitwalia uhuru wake, kwa matajiri
kuwatumia wanyonge kwa ajili ya mafao yao binafsi, huku wakiwaacha katika mateso na
hali ya kukata tamaa. Umefika wakati wa kutubu na kujipatanisha na nafsi pamoja na
jamii inayowazunguka ili kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Watu wajenge tabia
ya kusema na kusimamia ukweli unaowaweka huru badala ya kuendekeza majungu na umbea
ambao kamwe si mtaji, kama ni hivi anasema Askofu mkuu Nzapailanga, wengi wangekwisha
kutajirika.
Waamini na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wanapaswa
kujielekeza zaidi katika mchakato wa: haki, amani, msamaha na upatanisho, ili kuwaelekeza
watu katika njia inayowaongoza katika maendeleo endelevu badala ya kuendelea kuogelea
katika vita na maafa kwa watu na mali zao. Watu wanahitaji maendeleo na wala si vita
na kinzani.
Askofu mkuu Nzapalainga anawataka wafanyabiashara wanaoendelea
kujitajirisha kwa kuuza silaha, wakumbuke kwamba, damu ya watu wasiokuwa na hatia
inawalilia. Hii ni changamoto hata kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inadhibiti
biashara ya silaha kimataifa ili kupunguza vita, migogoro na kinzani zinazoendelea
kuwa ni chanzo kikuu cha maafa na umaskini. Umefika wakati kwa waamini na watu wote
wenye mapenzi mema, kukimbilia neema, huruma na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa
njia ya toba, msamaha na upatanisho wa kweli unaotoka katika undani wa mtu, ili kwa
pamoja, wananchi wote kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, waweze kutembea katika
njia ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa!