Ziara ya Kardinali Leonardi Sandri nchini Ethiopia.
Kardinali Leonardi Sandri, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki,
yuko ziarani Ethiopia, kama mjumbe wa Papa katika maadhimisho ya kutimia miaka 50
tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia. Kati ya mambo mengine,
hotuba zake amekazia umuhimu wa kuwa na umoja kwa wafuasi wa Kristo , kuunda Kanisa
Moja Takatifu na la mitume.
Katika ziara hii aliyoianza Ijumaa tarehe 5 Desemba,
siku ya Jumamosi 6 Desemba, alishiriki Ibada ya Misa iliyosomwa kwa kufuata maadhimisho
ya Liturujia Kanisa la Alesandria la Ethiopia , iliyofanyika katika Kanisa Kuu la
Gheez, mjini Addis Ababa, Ibada iliyohudhuriwa pia na Nunsio wa Papa Ethiopia,Askofu
Mkuu Luigi Bianco, pamoja na Askofu Mkuu wa Addis Ababa, Askofu Mkuu Berhaneiesus
Souraphiel, na Maaskofu wengine , kutoka nchi za Mashariki ya Kati.
Baada ya
Misa, Kardinali alitoa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francis, Baraka ya Kichungaji,
na kukabidhi kwa Askofu Mkuu wa Addis Ababa, medali ya mwaka wa pili wa utawala wa
Kipapa wa Papa Francisko.
Na baadaye Kardinali Sandri, akifuatana na Nunsio
na Askofu Mkuu Mousie wa Upatriaki wa Mashariki mwa Ethiopia , walikutana na watu
mbalimbali katika maeneo waliyo yatembelea ikiwemo Hospitali ya Mtakatifu Luke,
inayomilikiwa na Baraza la Maaskofu wa Ethiopia, ambako Kardinali Sandri alitoa salaam
za Papa na mchango wa taasisi kadhaa, hasa kutoka Baraza la Maaskofu Italia, na
pia shukrani kwa namna ya kipekee kwa Shirika la Masista la Tamil Nadu (India) na
madaktari wa CUAMM wa Verona Italia, kwa huduma yao katika hospitali hiyo.
Aidha
Kardinali alikutana na vijana na Maskauti katika Parokia moja wakiwa na mchungaji
wao, ambako aliweza kusikiliza historia na shughuli za Taasisi, ambayo ni pamoja
shule uuguzi, ambako kuna vijana walio mafunzoni wapatao 600. Taasisi ambayo kwa
sasa ina umri wa miaka 14 tangu kuanzishwa.
Kwa siku ya Jumatatu, Kardinali
pamoja na mambo mengine ,alikwenda katika Seminari Kuu ambako aliweza kufanya majadiliano
na waseminaristi , Mapadre na Masista na wafanyakazi katika maeneo mbalimbali. Kati
ya maswali aliyoulizwa yalilenga zaidi katika ukweli wa kiekumeni na mazungumzo kati
ya nchini Ethiopia hasa katika mtazamo kwamba hivi karibuni pia alipata nafasi ya
kuandamana na Papa Francisko, katika ziara ya kitume huko Uturuki. Nchi hizi mbili,
Uturuki na Ethiopia zote zina idadi ndogo ya Wakatoliki wanaoisha kati ya idadi
kubwa ya waumini wa Kiislam . Na pia maswali mengine yalilenga katika kutafakari uhusiano
kati ya ethiopia na Eritrea, ambamo katika ngazi ya Kanisa, ni familia moja kubwa
ya kanisa la Alesanderia yenye kufuata liturujia ya gheez.Lakini tofauti za kisiasa
kwa mataifa haya mawili, zinafanya watu wanaishi kwa shida kubwa, kutokana na mtafaruko
huo. Kardinali katika majibu yake, ametoa wito kwa raia wa nchi hizi mbili , kutafakari
kwa kina nini maana ya kusihi kwa amani na utulivu, na warejee katika maridhiano na
amani.
Kardinali aliikamilisha siku ya Jumatatu kwa kushiriki adhimisho la
Ekaristi kwa ajili ya Siku Kuu ya Maria Mkingiwa dhambi ya asili.