2014-12-09 09:31:22

Ungeni mkono mchakato wa kupambana na utumwa mamboleo!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawapongeza viongozi wa kidini waliotia sahihi tamko la pamoja linalowawajibisha kimaadili kupambana kwa nguvu zote dhidi ya utumwa mamboleo unaojionesha kwa namna ya pekee katika biashara haramu ya binadamu, tamko ambalo limetolewa hivi karibuni mjini Vatican.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema kwamba, kila mwanadamu ameumbwa huru na Mwenyezi Mungu; jambo ambalo linapaswa kuendelezwa kwa kujenga na kudumisha mafao ya wengi, usawa na udugu kati ya watu. Utumwa mamboleo unaofumbatwa katika biashara haramu ya binadamu, kazi za suluba, ukahaba, biashara ya viungo vya binadamu, ndoa shuruti pamoja na mambo yote yasiyoheshimu na kuthamini utu na heshima ya binadamu, hayana budi kuchukuliwa kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Dr. Fulata Mbano-Moyo mjumbe kutoka Baraza ya Makanisa Ulimwenguni aliyehudhuria katika tukio hili anasema kwamba, utumwa mamboleo unawageuza watu ambao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kuwa ni bidhaa zinazokidhi tamaa za kimwili na nguvu kazi inayohitajika katika mchakato wa uzalishaji mali. Baraza la Makanisa ni kati ya wadau wakuu wanaotaka kuona kwamba, utumwa mamboleo unatoweka katika uso wa nchi.

Kwa miaka mingi kumekuwepo na mapambano dhidi ya utumwa mamboleo pamoja na watu kudai haki zao msingi kwa kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi na jinsia; mambo ambayo yanawanyanyasa utu na heshima ya binadamu. Changamoto kubwa iliyoko kwa wakuu wa dini mbali mbali duniani ni kuhakikisha kwamba, tamko hili linavaliwa njuga ili liweze kutekelezwa katika ngazi mbali mbali.

Tukio la kuutia sahihi kwa Tamko hili lilihudhuriwa na viongozi wanawake kadhaa, changamoto ya kuhakikisha kwamba, kweli utumwa mamboleo unafutika kutoka katika uso wa dunia kwa kuwa waathirika wakubwa zaidi ni wanawake na watoto. Makanisa wanachama ambayo bado hayaweka sahihi katika Tamko hili yanahimizwa kufanya hivyo mapema iwezekanavyo.

Baba Mtakatifu Francisko katika tukio hili alisema kwamba, Tamko hili ni tukio la kihistoria, linalowahamasisha wakuu wa dini kuchukua hatua madhubuti katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo ambao leo ni hii ni janga na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Ni janga linalogusa maisha ya watu: kiuchumi, kijinsia, kisaikolojia pamoja na kudhalilisha wahanga wa vitendo hivi vya kinyama.

Mtandao Mpya wa Uhuru Duniani unapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, utumwa mamboleo unakomeshwa kwa kung'oa mizizi, ili Jamii iweze kuwa ni mashahidi wa huruma ya Mungu na upendo kwa watu wote waliotumbukizwa katika utumwa mamboleo. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya millioni ishirini nukta tisa wametumbukizwa katika kazi za suluba sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaouzwa kama bidhaa katika soko la biashara haramu ya binadamu au wametumbukizwa katika biashara ya ngono.All the contents on this site are copyrighted ©.